Habari za Punde

Maalim Seif Azindua Kongamano na Muungano na Katiba



Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia katika uzinduzi wa kongamano la Muungano na mchakato wa mabadiliko ya katiba huko Eacrotanal Mjini Zanzibar

Hassan Hamad OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katu hawatowasaliti wananchi wa Zanzibar katika kutoa maoni ya uundwaji wa katiba mpya ya Tanzania.

Amesema viongozi wataheshimu na kutetea maoni ya wananchi wanatakayoyatoa kwenye Tume ya marekebisho ya katiba, na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa  maoni yao wakati utakapofika.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo huko Eacrotanal Mjini Zanzibar alipokuwa akizindua kongamano linalohusu Muungano na Mchakato wa mabadiliko ya katiba ya Tanzania lililoandaliwa na kituo cha huduma za sheria Zanzibar.

Amesema kila mtanzania atakuwa huru kutoa maoni yake, na kwamba  ni fursa muhimu kwa Wazanzibari kueleza kero zinazowakabili ndani ya Muungano, badala ya kukaa kimya na kusubiri maamuzi yasiyokuwa na mustakbali mzuri na nchi yao.

Makamu wa Kwanza wa Rais amekiri kuwepo kwa kero nyingi za Muungano ambazo zinahitaji kutatuliwa kwa haraka ili kupunguza malalamiko ya wananchi wa pande mbili za Muungano.

Amefafanua kuwa kwa sasa yapo mawazo mengi kuhusu muundo wa Muungano, lakini amesema ni vyema kila nchi kati ya Tanganyika na Zanzibar ikawa na mamlaka yake kamili, kisha uanzishwe Muungano wa mkataba kwa mambo ambayo nchi mbili hizi zitakubaliana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kituo cha huduma za sheria Zanzibar Profesa Chris Maina Peter amesema ni muhimu kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kuunda katiba yao, ikizingatiwa kuwa katiba zilizopita hazikuwashirikisha wananchi moja kwa moja.

Nae Mwakilishi wa Shirika la Ford Foundation kanda ya Afrika Mashariki bwana Maurice Makoloo amesema shirika lake ambalo limekuwa likisaidia miradi mbali mbali ikiwemo kukuza demokrasia na kupunguza umaskini, litaendelea kushirikiana na Tanzania katika mchakato wake wa mabadiliko ya katiba ili kutimiza lengo lake la kukuza demokrasia katika nchi za Afrika Mashariki.

3 comments:

  1. Maalim Seif haina haja ya kusema pauro ni kijiko kikubwa sema tu ni pauro, kwa hiyo sema tu wananchi wa zanzibar hawautaki muungano waachiwe wapumueeeeeeeeeeeeeeeeeee.

    ReplyDelete
  2. Maalim Seif, wacha kutusemea Wazanzibari suala nyeti kama hili, ikiwa mumetushirikisha katika kuleta serikali ya umoja wa Kitaifa kwanini leo hamutaki kutushirikisha namna ya Muungano tunaoutaka. munajua wazi kuwa Wazanzibari hawana haja tena na Muungano. Tupeni Kura ya maoni kama ni vidume kweli.

    ReplyDelete
  3. Ndio maana sisi wengine tumejitoa CUF kwa sababu ya huyu mzee na chama chake.

    Jambo la msingi ni kuwarejeshea kadi zao kabla ya 2015. naamini kutokana na nguvu alizonazo ustadh Faridi anauwezo wa kuanzisha chama!
    Shime ndugu zangu tuikataeni CUF!!!!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.