Habari za Punde

Mwanamichezo Bora Tanzania Kuzoa 12 m/-

MWANAMICHEZO wa Tanzania atakayeibuka kuwa bora kwa mwaka 2011, atatia mikononi kitita cha dola elfu nane za Kimarekani (zaidi ya shilingi milioni 12 za Tanzania).

Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Imani Lwinga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema uamuzi huo unalenga kumpa uhuru mshindi aweze kufanya mambo anayoyapenda kutokana na zawadi hiyo.

“Mara hii tumeamua kutoa kitita hicho kwa kuamini kitakuwa changamoto ya kutosha kwa mwanamichezo atakayeshinda, ili ajisikie thamani aliyonayo na kujua kuwa kweli amepata kitu”, alisema Lwinga.

Aidha alifahamisha kuwa, kampuni yake iliombwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kinachoandaa tuzo hiyo, kwamba safari hii kuwe na mabadiliko kwa mshindi, akabidhiwe fedha badala ya zawadi ya gari kama ilivyokuwa mwaka jana, pamoja na cheti na kikombe.

Mbali ya donge hilo nono, Lwinga alisema Serengeti pia itatoa zawadi ya shilingi milioni moja kwa kila mshindi wa michezo mbalimbali, ambazo zitatolewa katika sherehe hizo zilizopangwa kufanyika Juni 14, mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee.

Naye Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alisema wanatarajia wanamichezo mbalimbali watapewa tuzo siku hiyo na kutaja michezo ambayo husika kuwa ni riadha, wavu, netiboli, kuogelea, tenisi, judo, kikapu, soka, ngumi za kulipwa, ngumi za ridhaa, gofu ya ridhaa, gofu ya kulipwa, baiskeli na kriketi.

Michezo mingine ni mpira wa mikono, Olimpiki maalum, mchezaji bora wa nje anayecheza Tanzania, mchezaji bora chipukizi, mchezaji bora wa Tanzania anayecheza nje, karate, mwanamichezo bora wa Tanzania mwaka 2011 na tuzo ya heshima.

Mhando ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Tuzo, alisema majina ya wanamichezo wote watakaowania tuzo hiyo watatangazwa kesho, na kuipongeza Serengeti kwa udhamini wao wa kila mwaka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.