Serikali imeeleza kuwa utekelezaji wa sharti la upendeleo kwa wazawa ndani ya Mfumo wa NeST linatarajiwa kuanza Julai, 2025.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Dkt. Ritta Enespher Kabati, ambaye alitaka kujua mkakati wa Serikali wa kuzijengea uwezo kampuni za ndani kwa kuzipa tenda za bilioni 50 kutokana na Sheria ya Ununuzi ya kuruhusu kupewa tenda zenye thamani ya sh. bilioni 20.
Alisema kuwa kwa sasa Timu ya ujenzi wa Mfumo wa NeST inakamilisha ujenzi ndani ya Mfumo, namna ya kutekeleza masuala ya upendeleo kwa wazawa.
“Mfumo wa NeST, kuna kategoria mbalimbali za wazabuni ambapo Kampuni itatambuliwa na Mfumo wa NeST kama kampuni ya ndani endapo: kampuni hiyo imesajiliwa Tanzania; inamilikiwa na raia wa Tanzania kwa asilimia 100 au raia wa Tanzania anamiliki mtaji wa hisa katika kampuni hiyo zisizopungua asilimia 51”, alibainisha Mhe. Chande.
Mhe. Chande alifafanua kuwa Kifungu cha 57 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya mwaka 2023, na Kanuni ya 45 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024 zimetenga zabuni za hadi shilingi bilioni 50 kwa ajili ya wazawa na Kampuni za ndani.
Aliongeza kuwa Kifungu cha 61 cha Sheria hiyo, kinaelekeza watu au kampuni binafsi kama hazina uwezo wa kutekeleza mikataba kuingia katika ushirika kwa lengo la kuimarisha uwezo.
No comments:
Post a Comment