Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali wakati wa Kikao cha
41 cha Mkutano wa 19 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 6 Juni 2025.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis
Hamza Khamis amesema si kila changamoto ni za Muungano, zipo zingine ambazo ni
za kisekta zinazotakiwa kujadiliwa na kutatuliwa na sekta zenyewe.
Amesema endapo sekta zimekutana na zikashindwa kufikia muafaka changamoto hizo zinawasilishwa katika Ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia Muungano ambapo wataalamu wanazijadili kisha makatibu wakuu, mawaziri na mwisho zinatatuliwa kupitia vikao vya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungani wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Naibu Waziri Khamis alisema hayo wakati
akijibu maswali ya Mbunge wa Mwera Mhe. Zahor Mohammed Haji bungeni jijini Dodoma leo tarehe 6 Juni 2025 aliyetaka kujua ni vigezo gani Serikali inaweka kutambua
changamoto za Muungano.
“Ili iitwe changamoto ya Muungano na kuingizwa kwenye orodha ya hoja za Muungano ni lazima iwe na uzito na kujadiliwa kama nilivyosema awali ikija kwenu inapitia kwenye hatua mbalimbali na hatimaye kwenye Kamati ya Pamoja ya Serikali zote mbili chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais,” alisema.
Aidha, Mhe. Khamis alisema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hoja za Muungano zilizosalia kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, makongamano, mijadala na vitabu vilivyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kwa upande mwingine, alisisitiza kuwa Muungano ni wa nchi
mbili, hivyo kuna umuhimu wa pande hizo kukaa pamoja na kujadili changamoto
zinapojitokeza ndio maana huchukua muda mrefu kuzitatua.
Alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni
Mhe. Tarimba Abbas aliyeuliza kama Serikali haioni haja ya kutatua haraka
changamoto kwani ina uzoefu mkubwa hasa ukizingatia ni miaka 60 sasa tangu
kuasisiwa kwa Muungano.
Awali akijibu swali la msingi la Mhe. Zahor, Naibu Waziri
Khamis alisema taarifa ya utekelezaji wa ufumbuzi wa changamoto za Muungano
inatarajiwa kutolewa kwa umma mara baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wake.
Alisema hayo wakati akijibu swali
la mbunge kuhusu ni lini Serikali italeta muswada wa sheria kuhusu changamoto
za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi ili sasa ziwe kwa mujibu wa sheria.
Naibu Khamis alisema katika kikao
cha Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ kilichofanyika tarehe 4 Aprili, 2025 Ikulu Dar
es Salaam kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto za Muungano kilitoa maelekezo
kwa Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa SJMT na SMZ kufanyia kazi jambo
hilo.
No comments:
Post a Comment