Habari za Punde

Mambo ya kufanya siku ya 'ArafahNa Abu Ammaar

Ndugu yangu katika Imani, siku ya kesho ni siku adhimu. Ni siku ya ‘Arafah. Kesho si siku ya kupamba nyumba, Kesho si siku ya kupika mapochopocho na mahanjumati. Kesho si siku ya kufanya shopping na kununua vitu, Kesho si siku ya raha au siku ya mapumziko.

Kesho ni siku bora kabisa katika masiku ya dunia hii ya Ar Rahmaan.

Ni siku ambayo Allaah Subhaanahu Wata’ala ameifanya tukufu, ni siku ambayo Allaah Subhaanahu Wata’ala amejitoa kwa Malaika na kuwaambia Malaaikah wawaangalie Mahujaji waliosimama ‘Arafah na kuuliza wanataka nini watu wangu hawa? Ni siku ambayo Allaah Subhaanahu Wata’ala atawaachia huru waja wake na moto mkali wa Jahannam. Ni siku ya kujitahidi katika kufanya ibada hili ndilo jambo la msingi tunalopaswa kulizingatia kesho na si kitu chengine chochote.

Nini tufanye kesho kwenye siku bora ya dunia?.

 Lazima tuhakikishe tunaitendea haki yake inayostahiki mpaka kuitwa siku bora ya dunia

1 Lala mapema siku ya leo ili kesho ukiamka uwe na nguvu za kutosha kwa ajili ya Ibada.

2 Tia nia ya kufunga siku ya ‘Arafah usiku( kwa funga za Sunnah inajuzu pia kutia nia asubuhi endapo utakuwa hujafanya jambo la kufunguza)

3  Ikiwezekana amka usiku na kusali Tahajjuud/Qiyaam Llayl japo kidogo kadri ya uwezo wako ila usijichoshe sana.

4 Kabla ya Alfajiri jihimu sana kufanya Istighfaar kwa kusema AstaghfiruLLaah kwa wingi ili uandikwe miongoni waliokuwa wakistaghfiru wakati wa usiku mkubwa.

5 Sali Alfajiri Jamaa msikitini (kwa wanaume, wanawake wasali majumbani mwao)

6 Baada ya kutoa salaam kumaliza sala ya Alfajiri anza kusoma takbiiraat kwa kusema: Allaahu Akbar, Allaahu Akbar, Laa Ilaaha Illa LLaahu wallaahu Akbar, Allaahu Akbar Walillaahil hamd kwa uchache mara tatu.

7 Bakia sehemu uliyosali alfajiri huku ukileta Takbir, Tahmid (Alhamdulillaah) na Tahlil ( Laa Ilaaha Illa Llaah) pia soma Qur’aan mpaka jua lichomoze, 

8 Jua litakapochomoza, Sali Rakaa mbili za Sunnah ya Shuruuq (kuchomoza kwa jua) Ukiyafanya haya malipo yake ni kama kuhiji na kufanya Umrah na Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam; 
    «من صلى الفجر في جماعة ثم جلس يذكر الله حتى تطلع الشمس ثم صلى ركعتين كتب له 
أجر حجة وعمرة تامة تامة» 
Mwenye Kusali Alfajiri Jamaa kisha akakaa na kumdhukuru (kumtaja) Allaah mpaka kuchomoza kwa jua kisha akasali rakaa mbili ataandikiwa ujira kama aliehiji na kufanya Umrah kikamilifu. Attirmdhiyy

9 Unaweza kupumzika kidogo huku ukijiandaa na kusali Sala ya Dhuhaa itakapingia wakati wake ambao ni pale jua litakapokuwa limeshachomoza na kumalizika kabla ya Adhuhuri. Tupo wengi hatujawahi kuisali sala hii tuitumie hii siku bora ya dunia kuanzia.

10 Sali Sala ya Dhuhaa – unaweza kuisali Rakaa mbili , au nne au sita au nane

11 Baada ya kumaliza Dhuhaa endelea na Takbir, Tahmid na Tahlil pamoja na kusoma Qur’aan.

12 Sali Adhuhuri Jamaa msikitini ( wanawake watasali majumbani), fanya takbir baada ya sala

13 Sikiliza Khutbatul Hajj ambayo hutolewa katika Masjid Namirah, katika viwanja vya ‘Arafah mjini Makkah siku ya mwezi Tisa ‘Arafah kupitia TV au hata simu yako ya mkononi na siku hizi hufasiriwa katika lugha tofauti kwani itakukumbusha katika siku hii Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam alitoa Khutba yake maarufu kama khutba ya kuaga ( Khutbatul Widaai)

14 Jiunge na Mahujaaj waliosimama ‘Arafah kwa kukithirisha duaa iliyo bora katika siku hii kwa kusema: Laa Ilaaha Ila Llaahu wahdahu Laa shariika Lahu, Lahul Mulk walahul hamd wahuwa ‘alaaa kulli Shay in Qadir

15 Sali Alasiri Jamaa Msikitini kisha endelea na Takbir, kisha fanya Tahmid na Tahlil pamoja na kusoma Qur’aan

16 Dua iliyo bora kabisa ni dua siku ya ‘Arafah hivyo katika siku hii bora kabisa muombe Allaah Subhaanahu Wata’ala kwa Ikhlas iliyokamilika huku ukitarajia Allaah Subhaanahu Wata’ala kuipokea dua yako kwamba siku hii jua lisitue ila na wewe uwe miongoni mwa waliosamehewa madhambi yao ya mwaka uliopita na mwaka utakaofuatia kama ilivyosema hadithi.

17 Pia kithirisha kumuomba Subhaanah akujaalie kuwa miongoni mwa wakatakaoachiwa huru na moto katika siku hii kama ilivyosema hadithi.

18 Sali Magharibi Jamaa Msikitini kisha futari na umshukuru Allaah Subhaanahu Wata’ala kwa kukuwafikisha kuweza kufanya ibada katika siku bora kabisa katika dunia, Pia muombe Allaah Subhaanahu Wata’ala azitakabalie ibada zako  kama vile aatakavyowatakabalia Mahujaji wanaotekeleza Ibada ya Hijja.

Allaahumma Amin

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.