Na Mwantanga Ame
MKE wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Suleiman Iddi, amewataka wazazi kupunguza tabia ya kuwapa mapenzi watoto yanayoshinda kuwakemea wanapofanya vitendo viovu na badala yake wawasimamie wawe na maadili mema.
Mama Asha alitoa rai hiyo jana wakati akifungua maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) yaliosomwa na Madrasa Muhlisina ya Donge Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.
Mama Asha, alisema hivi sasa kumezuka mtido wa baadhi ya wazee kushindwa kuwasimamia vyema watoto wao kuwa na maadili mema kunakosababishwa na kuwapa mapenzi kupita kiasi.
Alisema hali hiyo imeonekana zaidi kwa baadhi ya wazazi kuthubutu hata kuwapa vitu vya anasa ambavyo huchangia kufanya mambo maovu huku wakishundwa kuwakemea pale wanapotumia vibaya vitu hivyo.
Mama Asha alisema baya zaidi kuona hivi sasa baadhi ya awazazi hao wamekuwa hawana ushirikiano kwa wanaojitolea kusimamia maadili kwa vijana wakiwemo walimu katika skuli na vyuo vya madrasa.
Alisema hali hiyo ikiwachwa kuendelea inaweza ikasababisha hasara kubwa kwa taifa kutokana na kukuwa kwa vijana wataokuwa hawana maadili mema.
"Utaona siku hizi Mama anamfungia kibwebwe Mwalimu ati kampiga mtoto wake sasa tunawapa mapenzi kupita kiasi watoto jambo ambalo humuondoa woga wa kuendeleza vitendo viovu haya sio malezi tuliyolelewa" alisema Mama Asha.
Akiendelea Mama Asha, aliwaasa vijana kuacha kujiingiza katika vikundi vya watu wanaoashiria kutaka kuvuruga amani ya nchi.
Alisema wengi wa vijana hivi sasa wamekuwa wakijiingiza katika makundi ya watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi jambo ambalo hawafahamu hasara itayoweza kuwapata hapo baadae.
Mapema Mkuu wa kusimamia Vyuo vya Kur-ani Unguja na Pemba, Khamis Abduhamid, akitoa nasaha zake aliwaasa wazazi kujenga tabia ya kuwachunga watoto wao kutokana na kuanza kujitokeza viashiria vya maadili kushuka hasa kwa vijana.
Alisema tabia ya wazazi kuwaacha vijanaa kuwafunza mambo mema inaweza kuchangia kuwaoondoshea neema za Mwenyezi Mungu na katika maisha yao.

No comments:
Post a Comment