Habari za Punde

Wananchi Watoa Indhari kuhusu Bajeti. Wataka Mazingatio yawe Kuwapunguzia Wananchi Mzigo

Na Mwantanga Ame
WAKATI wananchi wa Zanzibar, wakisubiri kuanza kwa mjadala wa bajeti ya Zanzibar kesho, baadhi yao wamesema serikali itahitaji kuifanikisha kwa vitendo ili mipango ya maendeleo iliomo katika sekta tofauti iweze kufanikiwa.

Wananchi waliyaeleza hayo jana wakati wakizungumza na Zanzibar Leo kwa nyakati tofauti ikiwa ni hatua ya kutoa maoni yao baada ya bajeti hiyo kuwasilishwa Jumatano ya wiki iliyopita.

Walisema haja ya serikali kulitekeleza hilo ni moja ya jambo kubwa litaloweza kuleta mabadiliko katika maendeleo kwa vile bajeti ya mwaka uliopita ilionekana katika baadhi ya taassi hazikuweza kufanya vizuri.

Said Ahmeid Mkaazi wa Kikwajuni, alisema bajeti iliyopita iliweza kuifanya elimu ya juu kuingia dosari baada ya wanafunzi wengi walioomba kujiunga na masomo ya juu kukosa udhamini.

Hali hiyo alisema inaonesha wazi imetokana na fedha kidogo zilizoingizwa kwa ajili ya kuihudumia sekta hiyo jambo ambalo limesababisha vijana wengi kushindwa kuingia katika elimu ya juu.

Aidha, Mwananchi huyo alisema ingawa serikali imeamua kuongeza baadhi ya kodi lakini bado itapaswa kuona kodi za huduma ya kijamii ambazo bado hazijaelezwa hadharani kwa vile ziko katika sekta husika nazo zinahitaji kuona hazitamuongezea mwananchi mzigo wa maisha.

Akifafanua kauli yake hiyo alisema kodi ambazo huenda ikazipandisha kulingana na madiliko ya sheria ambazo serikali inakusudia kuzifanya ni pamoja na ya nyumba ambapo haitapaswa kuwekewa viwango kama zilivyo sasa kwa watu binafsi.

Alisema hilo wanapaswa kuliangalia kwa vile serikali haiko katika mfumo wa kufanya biashara na ipo kwa ajili ya kutoa huduma zaidi na haitakuwa busara kupandisha kodi kubwa kwa wakaazi wa nyumba za serikali.

Alisema jambo la busara kama ni suala nyumba hizo zinahitaji kufanyiwa matengenezo ni vyema ukaandaliwa mpango utaowahusisha wakaazi kutoa fedha kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati kwa kiasi kidogo cha fedha.

Alisema hilo litahitaji kuzingatiwa kwa vile si mara zote ada za posho la nyumba wananchi wanaopewa sio wote watumishi wa umma na huku watumishi wa umma kiwango wanacholipwa bado hakijawahi kuongezewa.

Aidha Mwananchi huyo alishauri, kwa serikali kuona inasimamia vyema baadhi ya maeneo ambayo wamepandisha kodi yakiwemo ya huduma ya mafuta kwa kuongeza asilimia 50 kwa kila lita jambo ambalo litahitaji kuangaliwa kwa wafanyabiashara kutopandisha kwa kiasi kikubwa bei ya bidhaa hiyo.

Alisema hilo linahitaji kuangaliwa kwa vile baadhi ya wafanyabiashara katika sekta ya usafirishaji wataanza kupandisha za bidhaa hizo kwa kisingizio cha kuongezeka kwa kodi.

Nae Mwananchi wa Kitope Abdalla Khamis akizungumza na Zanzibar Leo alisema bajeti iliyotangazwa juzi inaweza ikawa ni faraja kwa kuonyesha kuwa na mipango mingi ya maendeleo.

Alisema kitendo cha serikali kuweka utaratibu wa fedha zitazokuwa zikitolewa katika huduma zilizoongezewa kodi kuwarudia wananchi hasa katika sekta ya elimu ni mpango bora kwa vile nyingi ya skuli hivi sasa bado zinamatatizo ya kutokuwa na vikalio.

Alisema bado serikali inahitaji kuona michango inayotolewa kwa ajili ya elimu kuona inaiwekea taratibu nzuri zitazoiwezesha kutumika kwa faida ya skuli za watoto wanaochangia.

Kuhusu kuwashughulikiwa wazee Mwananchi huyo alisema ni jambo la busara kwani litaweza kupunguza tatizo la Wazee hao kuwa omba omba.

Bajeti ya Zanzibar iliyotangazwa juzi imeeleza kuwa uchumi wa Zanzibar kwa mwaka huu unatarajiwa kuimarika zaidi kutokana na mipango mbali mbali ya serikali katika ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo mbali mbali.

Katika bajeti hiyo SMZ imeweka maeneo ya vipaumbele kama afya, kuimarisha ajira kwa vijana, kuimarisha ustawi wa wazee, kuimarisha elimu, kuimarisha uchumi, pamoja na kuhifadhi mazingira na kukabiliana na tabia nchi.

SMZ katika bajeti yake mwaka huu imepanga kutumia shilingi bilioni 307, 797 milioni kwa kazi za kawaida na shilingi bilioni 341,147 milioni.

Aidha serikali inatarajia kukusanya shilingi bilioni 648,944 milioni.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.