Habari za Punde

Wawakilishi Mmekabidhiwa Majukumu Makubwa na Wananchi -- Spika Kificho

Na Himid Choko , BLW 
Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Mhe. Pandu Ameir Kificho amesema wajumbe wa Baraza hilo Wamekabidhiwa majukumu makubwa na wananchi hivyo ni lazima wawe na uelewa mpana juu ya mambo mbali mbali yanayohusu mustakbali wa maisha ya wananchi.

Mhe. Kificho ametaja baadhi ya majukumu hayo kua ni pamoja na utungaji wa sheria, kuidhinisha bajeti ya Serikali ya kila mwaka, kuihoji na kuidhinisha mipango ya maendeleo ya Serikali ambayo italenga matakwa ya wananchi kwa ajili ya maendeleo yao.

Mhe. Kificho amesema hayo leo wakati akifungua semina ya siku moja ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi iliyojadili Ripoti ya Wataalamu kuhusiana uwezo wa wajumbe katika masuala ya utungaji wa sheria na “Data Base” za Wadau wa Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi katika hoteli Ya Coconut Tree Village Marumbi, wilaya ya Kati , Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema kutokana na majukumu hayo mazito ni vyema kwa Wajumbe wa Baraza hilo kuwa na uelewa mpana katika mambo wanayo yasimamia.

Ameongeza kua iwapo wajumbe hawatakua na uelewa mkubwa wa masuala mbali mbali wanaweza kuidhinisha miradi au kutunga sheria ambazo hazitakua na maslahi kwa wananchi.

Hata hivyo Mhe. Spika ameyashukuru mashirika mbali mbali yanayofadhili mafunzo kwa Wajumbe hao hasa UNDP na kuyahimiza mashirika mengine kuiga mfano kama huo.

Katika hatua nyengine Mhe. Kificho amesisitiza haja ya kuimarisha mahusiano kati ya wajumbe mawaziri na wasiokuwa mawaziri katika kufanikisha majukumu ya Baraza hilo.

Akifafanua zaidi kuhusiana na suala hilo la mashirikiano Mhe. Spika amesema hatua hiyo haitaondosha wajibu wa Mwakilishi wa kuisimamia Serikali bali itazidisha uwajibikaji mzuri kwa Serikali.

Akiwasilisha Taarifa ya Utayarishaji kuhusu “Data Base” za Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi Mtaalamu Mwelekezi Dr. Moh’d Hafidh amesema matumizi ya Technolojia ya Habari na mawasiliano ni muhimu kwa wakati wa sasa, hivyo ni muhimu kwa wajumbe kujifunza technolojia hiyo.

Nae mtaalamu wa sheria Ndugu Stephen Mwenesi akiwasilisha ripoti yake kuhusu uwezo wa wajumbe katika masuala ya utungaji wa sheria amesema elimu zaidi bado inahitajika kwa wajumbe ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Kazi ya utayarishaji wa “Data Base” za Wadau wa Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi na tathmini ya uwezo wa wajumbe kuhusiana na masuala ya sheria inafadhiliwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la umoja wa Mataifa (UNDP) chini ya mpango wake wa kusaidia Mabunge Legislative Support Project (L.S.P).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.