Habari za Punde

KUZAMA MV. SKAGIT Tume Kuyatanzua Masuali Magumu

Na Gilbert Massawe
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, amesema Tume iliyoundwa na Rais ya kuchunguza kuzama kwa meli ya MV. Skagit itatoa majibu ya masuali magumu, likiwemo idadi kamili ya watu waliokuwemo kwenye meli hiyo.

Waziri huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, alipokuwa akijibu masuali ya Wajumbe wa Baraza hilo kufuatia serikali kuwasilisha taarifa rasmi za kuzama kwa meli ya MV. Skagit iliyotokea wiki moja iliyopita.

Waziri huyo alisema masuali magumu yaliyogubika kadhia nzima ya kuzama kwa meli hiyo, ikiwemo sababu ya kuzama kwake, itapatiwa majibu ya kuridhisha na Tume hiyo iliyoundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Aidha alisema ni matarajio ya serikali kuwa suali lililopo kuwa meli hiyo imeongezwa ukubwa tofauti na ule wa awali ilipotengenezwa nalo litachunguzwa na tume hiyo na kujulikana ukweli wake.

Waziri huyo alisema uwezo wa meli hiyo wa kusafiri katika maji kidogo kuliko ilivyokuwa ikifanya kazi nalo litachunguzwa kupatikana ukweli wake.

Waziri Aboud aliiagiza Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar kwa kushirikiana na Sumatra, kuzifanyia ukaguzi meli zote na zile zitakazothibitika kuwa zimechakaa na si salama kwa usafiri wa baharini zizuiliwe.

“Meli zote zinazosafirisha abiria zitafanyiwa uchunguzi na zile zitakazobainika kuwa chakavu zitazuiliwa na kwa hili tunawaomba sana wananchi wawe wavumilivu kwani hali hiyo itaathiri shughuli za usafiri”,alisema.

Alisema serikali inaangalia utaratibu mpya ambao utaruhusu meli ambazo zimetumika chini ya miaka 15 ndizo zitakazoruhusiwa kusafirisha abiria ili kuepuka athari zinazoendelea kujitokeza ambazo kwa kiasi kikubwa zainachangiwa na meli zilizochakaa.

Aliwaeleza wajumbe wa Baraza hilo kuwa serikali inajipanga kuhakikisha inanunua meli mpya, pamoja na kutoa kipaumbele zaidi kwa wawekezaji wenye kutaka kuingiza meli mpya.

Alisema serikali kwa kiasi kikubwa imejitahidi kutafanyiwakazi mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya kuzama kwa MV. Spice Islanders I, ikiwemo kuondoshwa kazini wale walioonekana kuzembea pamoja na baadhi yao kufikishwa mahakamani.

Katika hatua nyengine waziri huyo aliliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata watu wote wanaojishughulisha na uuzaji mikononi wa tiketi za usafiri wa baharini kwani jambo hilo limekuwa likisababisha kutopatikana kwa idadi ya wasafiri.

“Naliagiza jeshi la polisi kuwakamata wale wote wanaojishughulisha na uuzaji wa tiketi za usafiri wa baharini mikononi”,alisema waziri huyo.

Aidha waziri Aboud alivipongeza vikosi na vikundi vyote vilivyoshiriki kwenye zoezi la uokozi ambali linaendelea katika maeneo mbali mbali ya bahari.

Meli ya MV. Skagit ilizama Jumatano iliyopita ikitokea Dar es Salaam kuja Unguja ambapo hadi jana imetibitika kuwa watu 104 wamefariki dunia.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.