Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar imezifutia rasmi hati ya kufanya kazi Meli ya Mv.Kalama, Mv.Seagul na Mv.Sepideh kutokana na meli hizo kutokukidhi hali ya usalama wa abiria katika meli hizo.
Aidha meli hizo zimepewa muda wa mwezi mmoja kuanzia leo kuhakikisha zimeondoka katika maeneo ya Zanzibar kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi ya wamiliki wa Meli hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar Abdullah Husein Kombo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Afisini kwake kuhusu hali ya usafiri wa baharini na usalama Zanzibar.
Amesema Mamlaka hiyo imefanya tathmini na uhakiki wa kutosha na kujiridhisha kuwa Meli hizo hazifai kufanya kazi katika maeneo ya Zanzibar jambo ambalo limepelekea kuchukua hatua za kufuta hati za kufanyia kazi meli hizo.
Amefahamisha kuwa sababu kuu zilizopelekea Mamlaka kufanya maamuzi hayo ni pamoja na uchakavu,umri wa meli hizo kuwa mrefu na kupata matatizo mara kwa mara katika safari zao.
Kombo amefahamisha kuwa Sheria ya Mamlaka ya Usafiri na Bandari Zanzibar ya mwaka 2006 kifungu cha 17.1 inampa mamlaka Msajili wa Meli kuifuta meli yoyote ambayo itakuwa haikidhi usalama wa abiria.
Kufuatia sheria hiyo Kombo amesema watawataka wamiliki wa Meli hizo kuzirudisha hati za kufanyia kazi meli hizo ili waende kutafuta sehemu nyengine za usajili kinyume na maeneo ya Zanzibar.
Akizungumzia Meli ya Mv.Serengeti Kombo amesema wamelazimika kuiagiza meli hiyo kupunguza idadi ya abiria kutoka watu 800 hadi 350 na tani za mizigo kutoka 100 hadi 50 hadi pale ambapo watajiridhisha kutokana na hali ya meli hiyo ilivyo.
Aidha amegusia kuwa Kampuni ya Bakhresa italeta Meli kubwa ya abiria itakayofanya kazi zake Zanzibar ambapo pia Serikali ya Mapinduzi nayo iko mbioni kuhakikisha wanaleta meli inayokidhi mahitaji ya wananchi wa Zanzibar.
"Serikali ya Mapinduzi nayo iko mbioni kuhakikisha wanaleta meli inayokidhi mahitaji ya wananchi wa Zanzibar", tatizo letu kubwa sana Wazanzibari ni siasa nyingi. Miaka kadhaa hapo nyuma tulikuwa na meli ya MV Mapinduzi ambayo ililetwa ikiwa ni mpya kabisa baada ya kutengenezwa na Niigata Engineering Company ya Japan, ilikuwa ni imara sana na haikuwa ikuyumbishwa na mawimbi kwenye bahari yetu. Meli hiyo ilikuwa ikifanya safari zake Mtwara, Msumbiji hadi Komoro bila ya shida yoyote, lakini kwa kuwa tu ilikuwa ni milki ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kulifanywa juhudi za makusudi za kuisusiakwa maslahi ya kisiasa, yaani watu wasiitumie kwa lengo la kuikosesha serikali mapato kutokana na biashara hiyo ambayo kwa kweli ilikuwa ikitoa unafuu mkubwa sana wa bei kwa abiria wake. Ni ukweli ulio wazi kwamba watumiaji wakubwa wa meli zetu ni wananchi wa Pemba kuliko watumiaji wengine wowote, na hao ndio waliosusia kutumia meli za Shirika la Meli la Zanzibar mpaka kufikia Shirika hilo kushindwa kujiendesha kibiashara!! Kwa bahati mbaya sana meli za Shirika hili zilifanyiwa hata majaribio ya hujuma kwa kuingiza vyuma kwenye injini zake ili zife, washukiwa wa ufisadi hii hadi leo wapo wakiwa huru! Sasa leo tunapiga kelele eti serikali ilete meli, je tayari tumeshajirekebisha na tabia hizo zisizopendeza? Naomba tuwe wazi na matukio haya na tusifichane kitu. Kwa maoni yangu naoni serikali iache kujiingiza katika utoaji wa huduma hii.
ReplyDeleteSheikh hapa umekwenda mchomo au umeongea kwa jazba zaidi. Kama Mv. Mapinduzi ilikuwa ikitowa huduma mpaka Comoro kwanini ilishindwa kujiendesha au hata huko Comoro nako ni hao wapemba ndio waliokuwa wakiipanda? Mtwara pia nako ni wapemba tu? Sio kweli yeyote kuwa wananchi waliisusia meli kwa sababu za kisiasa. Kwa taarifa yako Mapinduzi ilishazeeka kama ilivyokuwa Maendeleo na zilikuwa zikipata hitilafu za mara kwa mara mpaka zikashindwa kwenda Mtwara ambapo soko lilikuwa kubwa la abiria na wafanyabiashara. Wapemba hawakuzisusia meli hizi hata hapo zilipokuwa chakavu, na kwa taarifa yako waliendelea kuzipanda kwani sio wote wenye uwezo wa kupanda speed boats. Lakini meli hizi zilishindwa kujiendesha kutokana na ufisadi na uongozi mbovu wa shirika la meli la Zanzibar na sio hizo sababu unazotaka tuamini.
ReplyDeleteNaomba ufanye tena research juu ya hili na utajuwa sababu hasa za kufa kwa meli zetu za Serikali kuliko kukurupuka na kuzusha yasiyokuwepo.