Mwashungi Tahir na Salmin Juma ZJMMC
WAZIRI wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mwinyihaji Makame Mwadini amesema katika kuthamini mchango wa watalii nchini Serikali imeamua kuanzisha kikosi maalum cha ulinzi ambacho kitaimarisha usalama wa watalii hao.
Amesema kikosi hicho kitakuwa na lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa watalii na mali zao ili wanapoingia nchini wasiwe na hofu juu ya usalama wao
Dk. Mwinyihaji ameyasema hayo kwenye ufungaji wa mafunzo ya kikosi kazi cha ulinzi na utalii huko katika viwanja vya polisi Ziwani mjini Zanzibar.
Alisema serikali ya Mapinduzi kupitia kwa Rais iko bega kwa bega kuona suala la Jeshi watalii linapewa nguvu ili kufanikiwa zaidi katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar.
“Watalii wanahitaji usalama wa mali zao na wao wenyewe hivyo jeshi hili linatoa matumaini mapya katika usalama wa watalii hao ambao watakaofika nchini “alisema waziri Mwinyihaji.
Amefahamisha kuwa utalii ni ushindani ambapo kabla ya kuja watalii nchini huulizia usalama ulivyo katika nchi husika na wakihakikisha kama upo usalama wa kutosha ndipo wanakuja kwa wingi.
Hivyo alisema usalama ni muhimu kwa mtalii katika kuhakikisha maishayao yanakuwa salama ili kuongeza moyo wa kuja zaidi nchini kwetu.
Nae Kamishna mkuu wa polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa alisema kuwa wameandaa jeshi hilo kwa makusudi ili kuhakikisha wanaondosha vitendo vya kihalifu na hatimae kukuza sekta ya utalii Zanzibar.
Pia alieleza mafunzo hayo yameendeshwa bila fedha kutoka kwa Serikali jambo ambalo linaonyesha moyo wa kujitolea kwa Jeshi hilo katika kujenga taifa bora.
Aidha aliiomba serikali kupitia Rais Ali Mohammed Shein kuwa bega kwa bega katika kutimiza malengo ya jeshi hilo.
Kwa upande wa risala ya wanafunzi ambao wamepatiwa mafunzo hayo wamesema wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vitendea kazi ikiwemo pingu ,simu, Kamera pamoja na usafiri ambao utawawezesha kufika katika matukio kwa wakati na kufanya kazi ipasavyo.
Mafunzo hayo ya kikosi kazi chaulinzi na utalii kimeanzishwa rasmi tarehe 12-5-2012 hadi kumalizika kwake tarehe 26-7-2012 mwaka huu na imewashirikisha jumla ya wanafunzi 123 , na kauli mbiu yao ni kazi kwa pamoja inawezekana.
No comments:
Post a Comment