Na Mwantanga Ame
WATOTO wa waasisi wa Chama cha Mapinduzi, wametajwa kuwa ni miongoni mwa wanaokusudia kuchukua fomu kuwania kiti cha Uwakilishi katika Jimbo la Bububu ambapo mchakato wake unaanza rasmi leo.
Uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu unafanyika baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo Mohammed Ali Mtondoo, kupitia tiketi ya Chama cha CCMdunia mapema mwaka huu baada ya kuuguwa maradhi ya kupooza mwili., kufariki
Kutokana na kifo hicho Tume ya Uchaguzi Zanzibar tayari imeitisha kufanyika kwa uchaguzi mdogo Septemba 16, mwaka huu ambapo wananchi wa Jimbo hilo watapiga kura.
Watoto wa waasisi tayari wametangaza nia hiyo baada ya kukutana na uongozi wa Chama katika wilaya ya Magharibi kuelezea nia yao ya kutaka kuchukua fomu katika zoezi.
Akizungumza na Zanzibar Leo Katibu wa CCM, wilaya ya Magharibi Unguja, Yahya Saleh, alisema ni kweli watu tisa watajitosa kuwania kiti hicho na shughuli hizo zitaanza rasmi leo asubuhi hadi jioni.
Akitaja majina ya wagombea hao ni pamoja na Hassan Ishau Khamis, Hussen Ibrahim Makungu, (Bhaa), Omar Ibrahim Kilupi, Khamis Abdalla, Fatma Adam, Iddi Makame na Subira Haji.
Katibu huyo alisema maandalizi kamili ya zoezi la uchukuaji wa fomu hizo tayari yamekamilika na kuanzia leo wagombea hao wataanza kuchukua fomu katika afisi za Chama wilaya ambapo kazi hiyo itakamilishwa ifikapo Jilai 28, mwaka huu.
Alisema Julai 29, mwaka huu, wagombea wataojitokeza kuchukua fomu watafikishwa katika mkutano mkuu wa maalum ambapo utaweza kutoa majina matatu bora kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo.
Alisema katika mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa rasmi la Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuia, ambapo utaweza kutoa majina matatu yatayofikishwa kwa wanachama wa CCM ili wagombea hao waweze kufanya kampeni zao zoezi ambalo litafanyika kuanzia Julai 31, 2012.
Alisema majina ya wagombea hao yatapigiwa kampeni katika matawi tofauti ya jimbo hilo likiwemo Bububu, Mwanyanya, Kibweni, Sharifu Msa na Kiboko yao.
Alisema zoezi la kupigiwa kura kwa wagombea hao linatarajiwa kufanyika Agosti 5, mwaka huu na baada ya kumaliza katika hatua hizo majina hayo yanatarajiwa kufikishwa katika vikao vya Chama kikiwemo cha Kamati ya Siasa ya Wilaya ili baadae kufikishwa katika vikao vya juu vya chama hicho.
Wakati hayo yakiendelea kutokea katika Chama cha Mapinduzi tayari baadhi ya vyama vya upinzani vimeanza kujigamba kuweka wagombea wataoweza kuchuana vizuri na mgombea wa Chama cha Mapinduzi.
Hapo awali Katibu wa Chama cha TADEA Zanzibar, Juma Ali Khatib, akizungumzia juu ya suala hilo alisema hawana sababu ya kutoshiriki uchaguzi huo kwani tayari kuna wanachama wengi wanaotaka kuwania nafasi hiyo na watahakikisha wanashinda ambapo kati ta wanachama watao wasimamisha wamo wanawake.
Mkurugenzi wa Sera wa Chama cha Wakulima na Wafanyabishara Zanzibar, AFP, Rashid Yussuf Mchenga, akizungumzia msimamo wa Chama hicho juu ya hilo, alisema tayari Chama chao kimeshafanya uteuzi wa Mgombea ataewania nafasi hiyo na wanahakikisha kuwa atashinda baada ya kumteuwa Mussa Ali Mussa na hivi sasa wameanza maandalizi ya kukamilisha taratibu za Tume ya Uchaguzi.
Upande wa Chama cha CUF kupitia msemaji wake Mkurugenzi Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma, Salum Bimani, akizungumza na Zanzibar Leo, nae alisema chama chao kitahakikisha uchaguzi huo unakuwa huru na haki na chama chao kitaibuka na ushindi ambapo mgombea wake wataanza kutafutwa Julai 14, mwaka huu.
Tume ya Uchaguzi imepanga kazi za uchukuaji na urejeshaji wa fomu zitaanza Agosti 22, 2012 hadi Agosti 30, mwaka huu na uteuzi wa wagombea utafanyika Agosti 30, mwaka huu huku kampeni zinatarajiwa kuanza Agosti 31, 2012 hadi Septemba 15, 2012 na uchaguzi utafanyika Septemba 16, 2012.
No comments:
Post a Comment