Habari za Punde

Wazalendo kutengenezewa ajira zaidi


Na Husna Mohammed
WAZIRI wa Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman amesema kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, itaongeza fursa zaidi za ajira kwa wazalendo.

Waziri huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akiwasilisha makadirio ya matumizi na mapato ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013.

Alisema katika kuifikia hatua hiyo, wizara yake itashirikiana na kamati za ajira za kitaifa ikiwemi mikoa na wilaya katika kujenga mikakati ya kutengeneza na kuwapatia ajira vijana wa Kizanzibari.

Aidha alifahamisha kuwa wataimarisha na kukipatia taarifa kitengo cha kukusanya ili kutoa taarifa za ajira, ambapo katika kufanilikisha hilo elimu ya ajira itatolewa kupitia njia mbalimbali.

"Tutaimarisha mashirikiano na taasisi za kitaifa kikanda na kimataifa katika masula yanayohusiana na ajira na kushirikiana na wizara ya Kazi na ajira ya Tanzania bara, Shirika la Kazi Duniani (ILO) pamoja na washirika wa masuala ya kazi", alisema.

Akizungumzia kuhusu malengo ya Kamisheni ya Kazi kwa mwaka 2012/2013, waziri Haroun, alisema wizara yake itasimamia utekelezaji wa sheria za kazi, sera na programu zinazohusu masuala ya kazi.

Aidha alisema wizara hiyo itawajengea uwezo katika usimamizi na utekelezaji wa mikakati ya kimataifa ya kazi na kuimarisha mfumo wa suluhisho na migogoro ya kazi.

Kuhusu usalama kazini Haroun, alisema serikali inakusudia kufanya marekebisho na kuimarisha mpango wa ukaguzi kwa ajili ya tathmini hali ya usalama na afya katika sehemu za kazi.

Aidha alisema pia serikali itaijengea uwezo Idara ya usalama na afya kazini kwa kuipatia vifaa vya kisasa na utaalamu ili kwenda sambamba na viwango vya kitaifa na kimataifa.

Hata hivyo, alisema serikali itafuatilia kwa karibu zaidi matukio ya ajali, maradhi na madhara yanayotokana na ajali katika sehemu za kazi pamoja na kuwekwa utaratibu bora wa wafanyakazi kuchunguzwa afya zao.

Mapema baadhi ya wawakilishi wakichangia bajeti hiyo, walisema kuwa taasisi binafsi ikiwemo mahoteli yamekuwa na ajiara nyingi zinazowahusu wageni kuliko wazalendo.

Walisema kuweko kwa hali hiyo kwa kiasi kikubwa kumekuwa kukiuka wageni kuwapa kipaumbele jambo ambalo linawakosesha fursa wenyeji kupata ajira.

Kuhusu migogoro ya kikazi wawakilishi hao walishauri Serikali kufatilia kwa kina mikataba ambayo mara nyingi imekuwa ikizuwa migogoro kati ya waajiri na waajiriwa jambo ambalo linawakosesha haki zao mara baada ya kuachishwa kazi kwa sababu zisizo za kimsingi.

Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa shilingi bilioni 2, 679,000,000 kwa kazi za kawaida.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.