Habari za Punde

CAG ayanyooshea kidole mashirika ya umma


Na Mwantanga Ame
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir amesema mashirika ya umma ndiyo yanayoongoza tatizo la kuchelewesha ufungaji wa mahesabu ya serikali kwa mwaka.

Waziri huyo alieleza hayo jana alipokuwa akiwasilisha ripoti mbili za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali Zanzibar kwa mwaka wa 2010/2011.

Waziri huyo alisema tatizo hilo linachangia kutoeleweka mwenendo wa shughuli zao wanazozifanya jambo ambalo linatatiza hesabu sahihi.

Alisema mashirika ya serikali yanashindwa kufunga mahesabu yake kwa wakati jambo ambalo limekuwa likiikwaza Ofisi ya mdhibiti kushindwa kufanya kazi zake kwa wakati.

Akitoa mfano wa mashirika hayo alisema ni pamoja na shirika la Umeme Zanzibar, Shirika la Meli na Uwakala, Shirika la Bima la Zanzibar, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Shirika la Huduma za Maktaba, Shirika la Utalii na Shirika la la Biashara la Taifa (ZSTC).

Akizungumzia kiwango cha uwekaji wa hesabu za serikali kwa wizara, alisema umeimarika kwa kiasi kikubwa hali inayosababisha taasisi hizo kufunga hesabu zake kwa wakati na mujibu wa sheria na kanuni za fedha.

Licha ya mafanikio hayo, waziri huyo alisema bado taasisi za serikali zitapaswa kuimarisha suala la uwekaji wa kumbukumbu za mahesabu ya serikali kwa kutumia madaftari ya hesabu pamoja na hifadhi na udhibiti ya vifaa na mali za serikali.

Waziri Kheir alisema Ofisi ya Mdhibiti, inashauri viongozi wakuu wa taasisi kuwa karibu na watendaji wao ili kufuatilia mwenendo mzima wa fedha kuanzia ukusanyaji, matumizi na uhifadhi wa raslimali za umma, ikiwa ni hatua itayoongeza utawala bora katika udhibiti wa mali za umma.

Alisema katika mwaka 2010/2011 mambo yaliyobainika ni pamoja na kuimarika juu ya suala la kuweka kumbukumbu huku kukiwa na dosari za kiutendaji likiwemo suala la kukosekana kwa maelezo kwa baadhi ya hoja.

Aidha, udhaifu mwengine uliobainika alisema ni matatizo katika ufungaji na uwasilishaji wa mahesabu katika mashirika kutokana na kuwepo kwa malimbikizo ya madeni wanayodaiwa au kudaiwa taasisi za serikali.

Tatizo jengine ni pamoja na kukosekana kwa baadhi ya vielelezo muhimu katika ukusanyaji wa mapato, kutofuatwa makubaliano ya mikataba na kutokuwapo kwa kumbukumbu za vifaa vinavyonunuliwa na serikali.

Akizungumzia upande wa miradi ya maendeleo waziri huyo alisema eneo hilo limebainika kuwepo kwa udanganyifu uliokuwa ukifanywa kwa miradhi hiyo kutoenda sambamba na hadhi ya fedha zilizotumika.

Alisema miradi hiyo ni ile iliyokuwa ikihusu shughuli za ujenzi wa bara bara, afisi za serikali, vituo vya afya, miundo mbinu ya maji safi na salama, huduma mbali mbali za elimu, ambapo ilionekana kushindwa kufikia malengo kulingana na fedha zilizotengewa.

Upande wa ukusanyaji wa mapato ripoti hiyo imeeleza kuwa, kwa kipindi cha mwaka 2010/2011 haukuweza kufikia malengo kwani fedha zilizokadiriwa kukusanywa zilikuwa ni silingi 236.730 bilioni lakini kilichokusanywa ni shilingi 219.058 bilioni.

Hata hivyo alisema waziri huyo ripoti hiyo imebaini bado kuna fursa nzuri ya kukusanya mapato zaidi iwapo jitihada za makusudi zitachukuliwa katika kuimarisha vianzio mbali mbali vya mapato vya ndani hasa katika sekta ya utalii.

Khusu fedha za matumizi ya kawaida Waziri huyo alisema kwa mwaka huo umeonesha kuwepo kwa mafanikio makubwa kwani yalifikia asilimia 96.7 ya makadirio yaliopangwa.

Waziri huyo pia alisema upande wa matumizi ya maendeleo serikalai ilijipangia kutumia 39.4 bilioni kwa matumizi hayo baada ya kuingiziwa shilingi 30.485 bilioni ikiwa ni sawa na asilimia 77.37 ya makadirio.

Alisema kwa upande wa washirika wa maendeleo serikali ilijipangia kutumia shilingi 211.804 bilioni, ambapo fedha zilizoingizwa kwa shughuli hizo ni bilioni 136.27 ikiwa ni sawa na asilimia 64.3 ya makadirio.

Waziri huyo, akizungumzia juu ya suala la utunzaji wa thamani ripoti hiyo imebaini nako kuna matatizo makubwa ya kutotambulika mali hizo, kuzitunza pamoja na kuziwekea kumbukumbu jambo ambalo linasababisha kupote bila ya kutambulika.

Kutokana na hali hiyo Waziri huyo alisema kunahitaji kuona serikali inakabiliana na changamoto mbali mbali zitazoweza kuondoa matatizo yaliojitoikeza ndani ya ripoti hizo likiwemo suala la kwenda sambamba na mabadiliko ya mifumo na viwango vya kitaifa na kimataifa vya uwekaji wa kumbukumbu za mahesabu pamoja na ufungaji wake.

Alisema taasisi ya mdhibiti hapo baadae inakusudia kuona inaimarisha ushahijishajiusimaizi, uwazi na uwajibikaji wa masuala ya fedha na mali ya umma kwa kushirikiana na taasisi nyengine.

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya PAC, Fatma Mbarouk Said alisema ni busara kwa serikali kuthamini nguvu na gharama kwa vile uandaaji wa ripoti hizo unatumia fedha za walipa kodi wa nchi wa Zanzibar.

Alisema ili kujinusuru na upotevu wa fedha kutokea uzembe, vyenginevyo maoni hayo yasipozingatiwa basi ni dhahir kutaongeza hasara isiyo na sababu na inayoepukika.

Alisema miongoni mwa mambo yaliyomo kwenye ripoti hizo za Mkaguzi Kamati hiyo, inatakiwa kuyafuatilia ni yale yanayohusiana na miradi ya ujenzi, mambo mengine ni ya manunuzi ya dawa za kutibu binaadamu na wanyama pamoja na fani nyengine za kitaalamu.

Kutokana na hilo Makamu Fatma alisema Kamati hiyo inaliomba Baraza hilo kutenga fungu maalum kwa ajili ya kukodi wataalamu wa fani hizo ili waweze kuisaidia katika kazi zake badala ya kuwa na mtaalamu wa fani ya ukaguzi pekee.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.