Habari za Punde

Mbio za kampeni Bububu kuanza leo. CCM, CUF kuwatoa kiukumbi wagombea wake

Na Mwandishi wetu
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mohamed Gharib Bilal, anatarajiwa kuzindua kampeni za CCM za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema kuwa uzinduzi wa kampeni hizo utafanyika uwanja wa mpira kwa Geji uliopo Kijichi wilaya ya Magharibi, Unguja.

Alisema katika uchaguzi huo, Chama cha Mapinduzi kimemsimamisha Hussein Ibrahim Makungu (39) na kuwataka viongozi na wanachama wa Chama hicho jimboni humo kuhakikisha wanaleta ushindi usioshaka ili jimbo hilo liendelee kuwa chini ya himaya ya Chama hicho.

Uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu unafanyika kufuatia aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo hilo Salum Amour Mtondoo kufariki dunia Machi 15, mwaka huu, baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa shindikizo la damu.

Vuai alisema maandalizi ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu yamekamilika baada ya mgombea wa chama cha Mapinduzi kupata ridhaa ya Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa kuhalalishwa kuwa mgombea asiye na matatizo.

“'Tumejiandaa kutetea jimbo letu la Bububu kwa kishindo ambapo maandalizi ya kampeni za uchaguzi huo yamekamilika kwa asilimia mia moja huku mgombea wetu akikubalika na wapiga kura”, alisema Vuai.

Katika uchaguzi huo vyama 10 vinashiriki ikiwemo CCM, CUF, AFP, SAU, Jahazi asilia, pamoja na NCCR-Mageuzi, TADEA, NRA, UPDP, huku chama kipya kilichopata usajili cha ADC kikishiriki kwa mara ya kwanza katika harakati za siasa.

Hata hivyo, chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA kimeshindwa kujitosa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mdogo jimbo la Bububu huku msaidizi katibu wake aliyefahamika kwa jina la Dadi akisema kwamba wametafakari na wameona ni bora wasishiriki katika uchaguzi huo.

Kampeni hizo zitakazochukuwa wiki mbili zitahitimishwa na kufungwa na mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi Septemba 15 katika uwanja wa Aljazeera huko Bububu.

Ofisa wa uchaguzi wilaya ya Magharibi Unguja wa tume ya uchaguzi (ZEC) Ali Rashid Suluhu alivitaka vyama vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo kufuata maelekezo na masharti ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria ikiwemo kutumia lugha nzuri katika majukwaa ya mikutano ya kisiasa.

Katika hatua nyengine Chama cha CUF kimeeleza kuwa nacho kitashuka katika kiwanja cha skuli ya Bububu kuzindua rasmi kampeni za kuliwania jimbo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Haki za Binaadam Habari na Mahusiano ya Umma, Salim Bimani alieleza kuwa mkutano wa kumtambulisha mgombea wa Chama hicho Issa Khamis Issa utazinduliwa na Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali.

Bimani alisema mkutano huo utaanza majira ya saa 8 mchana ambao pia utahudhiuriwa na viongozi mbali mbali wa kitaifa wa Chama hicho.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.