Habari za Punde

Ziara ya kuhamasisha utalii kwa wote

Mkuu wa huduma za Elimu ya Makumbusho Zanzibar Ramadhan Machano akizungumza na Wawakilishi wa vikundi vinavyofanya mazoezi ya viungo Zanzibar hawapo pichani katika Makumbusho kuu ya Taifa Baitil elajaib


Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 

 Washiriki ambao wameenda kuzuru katika maeneo tofauti ya makumbusho ya Taifa ya Zanzibar wametakiwa kuwa Mabolazi wazuri katika jamii zao ili kuhakikisha kuwa jamii ya Zanzibar inajenga utamaduni wa kutembelea katika makumbusho hayo. 

 Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa huduma za Elimu ya Makumbusho Zanzibar Ramadhan Machano katika ziara yake na Wawakilishi wa Vikundi vitano vinavyofanya mazoezi ya viungo Zanzibar kwa lengo la kuhamasisha utekelezaji wa mpango wa Utalii kwa wote. 


 Amesema wameamua kuwaalika wawakilishi hao kutembelea maeneo ya makumbusho ya Zanzibar ili wasaidie kuwahamsisha wananchi kutembelea maeneo hayo kwa lengo la kujua historia ya Zanzibar. Machano amefahamisha kuwa,kwa vile wawakilishi hao wanajumuika na jamii kwa ujumla anaamini kuwa wanaweza kuibadili jamii na kuepukana na dhana iliyojengeka kwa wananchi wengi kuwa utalii unafanywa na Wageni. 

 Aidha amefahamisha kuwa kufanikiwa kwa Mpango wa Utalii kwa Wote kutaiwezesha Idara ya Makumbusho kutokutegemea wageni katika kupata mapato yake badala yake Wenyeji wanaweza kuchukua jukumu hilo. 

 Machano ametaja kingilio ambacho wenyeji wanapaswa kuchangia wanapofika katika maeneo ya Makumbusho kuwa ni Shilingi 1,000 kwa mtu mzima na mtoto Shilingi mia tano. Aidha Machano amesema wataendelea kuwashirikisha viongozi wengine ikiwemo Mashekh na Walimu wa Shule ili waweze kuisaidia Serikali katika kuhimiza utalii kwa wote. 

 Kwa upande wao washiriki wa ziara hiyo wamemuahidi Mkuu huyo kuwa Wataendelea kuwahamasisha wanachama wao na jamii kwa ujumla ili waweze kutenga muda wao kwa lengo la kutembelea maeneo ya makumbusho. 

 Wamesema wamejifunza mengi katika ziara hiyo ikiwemo kujua asili ya utamaduni wa Mswahili sambamba na kujionea uhalisia wa mambo kinyume na kusimuliwa katika vitabu vya kihistoria. Ziara hiyo ambayo ilijumuisha vikundi vya Kata Presha, New Generation, Obama, Nameless na Mandela ilianzia katika Makumbusho kuu ya Taifa Baitil Ajaib na kuendelea katika Magofu ya Mwinyimkuu Dunga, Bi Kihole-Bungi na kumalizia katika Pango la Kuumbi-Jambiani.

 IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 01/09/2012

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.