Mjini Zanzibar,akifuatana na ujumbe wa Watu kumi na moja (11) leo. [Picha na Ramadhan Othman Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Afya Jimbo la Jiangsu ncini China Bibi Wong Young Hong,(kushoto) alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,akiwa na ujumbe wa Watu kumi na moja (11) leo.
[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.]
[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.]
Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa unaoshighulikia sekta ya Afya kutoka Jimbo la Jiangsu nchini China, ambapo ujumbe huo uliahidi kuendelea kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya.
Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu mjini Zanzibar ambao ujumbe huo wa watu kumi na mojam kutoka Jimbo la Jiangsu uliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afya wa Jimbo hilo Bibi Wang Yonghong.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alitoa pongezi na shukurani kwa China kutokana na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya.
Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati yake na China hasa katika sekta ya afya ambapo Zanzibar imeweza kufaidika kwa kupata madaktari wataalamu kutoka nchi hiyo.
Alisema kuwa mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 China ilikuwa ni nchi ya mwanzo kuiunga mkono Zanzibar katika kusaidia kuimarisha sekta za maendeleo na ndipo ilipoanza kuleta kundi la madaktari 24 hapa Zanzibar ambao walifanya kazi katika hospitali ya Abdalla Mzee huko Pemba na MnaziMmoja Unguja.
Kutokana na msaada huo, Dk. Shein alilipongeza Jimbo la Jiangsu kwa kuendeleza utamaduni wa kuleta madaktari kwa kila baada ya muda ambapo tayari makundi 24 ya madaktari wameshafika na kufanya kazi hapa nchini na kuweza kutoa huduma za afya ambazo zimeweza kupendwa na kuthaminiwa sana na wananchi kutokana na ubora wake.
Aidha, Dk. Shein alitoa salamu za shukurani kwa uongozi wa Jimbo hilo kwa kusaidia kuimarisha sekta hiyo ya afya ambayo mbali ya kuleta madaktari pia, Zanzibar imeweza kupata misaada ya dawa, vifaa mbali mbali pamoja na mafunzo kwa madaktari wazalendo nchini China.
Dk. Shein pia, hakuacha kutoa pongezi na shukurani kwa uongozi huo kutokana na kutekeleza ahadi zake mbali mbali inazozitoa katika kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kusaidia mashine maalum ya upasuaji ya kisasa hali ambayo itatoa huduma kwa wananchi wa Zanzibar na wanao toka nje ya Zanzibar.
Katika huduma itakayotolewa kwa kutumia mashine hiyo mgonjwa atafanyiwa upasuaji kupitia kwenye kioo maalum bila ya kupasuliwa (Minimal Invesive Surgery).
Miongoni mwa faida kubwa ya mashine hiyo ni pamoja na kumpunguzia maumivu mgonjwa na kupunguza siku za kulala hospitali, jambo ambalo pia, linapunguza gharama za kumhudumia mgonjwa pamoja na gharama za kuwasafirisha wagonjwa nje ya nchi.
Dk. Shein aliueleza ujumbe huo kuwa azma yao ya kuifanyia ujenzi mkubwa hospitali ya Abdalla Mzee ilioko kisiwani Pemba ambapo mchakato wake umeanza itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar na kutoa huduma kwa jamii.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa hatua za kuisaidia ana kuendelea kuiunga mkono hospitali ya MnaziMmoja kwa kuisaidia vifaa, wataalamu pamoja na vitengo vyake vyengine kutasaidia lengo la serikali la kuifanya hospitali hiyo kuwa ya rufaa.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliueleza ujumbe huo kuwa miongoni mwa malengo ya serikali anayoiongoza ni kuanzisha kitengo cha kutoa huduma za utibabu wa maradhi ya saratani, huduma za utibabu wa maradhi ya figo na maradhi ya moyo, hivyo kuwepo kwa mashirikiano katika sekta ya afya na Jimbo la Jiangsu kutaharakisha azma hiyo.
Nae kiongozi wa ujumbe huo Bibi Wang Yonghong, alimueleza Dk. Shein kuwa Mbali na misada hiyo iliyoitolewa bado Jimbo la Jiangsu litaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya na kuhakikisha Zanzibar inatajika katika sekta hiyo.
Aidha, Bibi Yong hong alieleza kuwa pia, wamo katika mchakato wa ujenzi wa kituo cha wenye matatizo ya kupasuka kwa midomo katika hospitali ya MnaziMmoja.
Pia, Bibi Yonghong alimtambulisha Professa, Dk. Yin Changjun kutoka katika Idara inayoshughulikia maradhi ya mkojo (Urological Department) katika jimbo la Jiangsu ambaye atasaidia kutoa huduma katika hospitali ya MnaziMmoja pamoja na mafunzo kwa madaktari wazalendo kutokana na uzoefu mkubwa alionao Profesa huyo.
Mkurugenzi huyo Mkuu pia, alitoa salamu kutoa kwa viongozi wa Jimbo hilo na kumfikishia Dk. Shein huku akipongeza uhusiano na ushirikiano uliopo.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk. Jidawi, alimueleza Rais jinsi jimbo la Jiangsu lilivyo na mahusiano na mashirikiano mema na Zanzibar katika kusaidia kuimarisha sekta ya afya hapa nchini jambo ambalo linahistoria ya muda mferu.
No comments:
Post a Comment