Habari za Punde

Waziri amrejesha kazini Katibu ZFA

Apinga mamlaka yake kukiukwa, kutoshauriwa

Na Salum Vuai, Maelezo

KATIBU Mkuu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Kassim Haji Salum, ametakiwa kurudi kazini mara moja, siku kadhaa baada ya kusimamishwa na uongozi wa chama hicho kwa madai mbalimbali.
 
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk, mbele ya viongozi wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) na watendaji wengine wa wizara yake juzi.
 
Waziri huyo alieleza bayana kuwa hatambui uamuzi wa ZFA kumsimamisha kazi Katibu huyo, akisema umekiuka mamlaka aliyopewa kama Waziri, kuteua Katibu baada ya kushauriana na uongozi wa juu wa chama hicho.
 
Katibu Mkuu wa BTMZ Hassan Tawakal Khairallah, ameliambia gazeti hili kwa niaba ya Waziri huyo kuwa, katiba ya ZFA vifungu 42 na 43, vinampa uwezo Waziri kuteua Katibu kwa kushauriana na Rais wa ZFA, jambo ambalo alilitimiza.  
 
Hata hivyo, alisema, Waziri alilazimika kushauriana na Makamu wawili wa Rais, Pemba na Unguja, kwa kuwa wakati huo ZFA haikuwa na Rais baada ya kujiuzulu kwa Ali Ferej aliyekuwa akikalia kiti hicho.
 
Khairallah alifahamisha kuwa, Waziri hakufanya hivyo kwa sababu ya kumtetea Kassim, kwani yawezekana akawa amefanya makosa aliyodaiwa, lakini kabla kumsimamisha, ZFA ilipaswa kumuona Waziti kwa mashauriano, kama ambavyo walifanya awali wakati wa kumpendekeza kupewa wadhifa huo.
 
Aidha, imebainika kuwa, kifungu cha 93 ambacho ZFA imekitumia kumsimamisha Kassim hakina mashiko, kwani kinarejea kifungu cha 92, ambacho  hakizungumzii mtu aliyesimamishwa bali kinataja mtendaji au kiongozi anayejiuzulu.
 
Mbali ya kasoro hiyo, mapungufu mengine kadhaa yamebainika katika katiba ya ZFA, na hivyo Waziri amekitaka chama hicho kikae na kuipitia upya katiba yake, kwa ajili ya kuifanyia marekebisho ili iweze kufanya kazi vyema.
 
Zaidi ya wiki moja iliyopita, Rais wa ZFA Amani Ibrahim Makungu, ambaye sasa yuko safarini nje ya nchi, alimsimamisha kazi Katibu Mkuu Kassim Haji Salum kwa madai mbalimbali ikiwemo kuvujisha siri za chama, kukosa uaminifu na kutokuwa na taaluma ya kompyuta ambayo ni muhimu kwa mawasiliano ya kikazi na wadau wa chama hicho. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.