Na Mwajuma Juma
MIKOA mitano ya Zanzibar imethibitisha kushiriki michuano ya Taifa ya mchezo wa riadha yatakayoanza keshokutwa Septemba 7, mjini Dar es Salaam.
Katibu wa Chama cha Riadha Zanzibar (ZAAA) Khamis Gulam, amemwambia mwandishi wa habari hizi kuwa, michuano hiyo itakayoshirikisha mikoa yote ya Tanzania, itadumu kwa siku tatu, na kwamba washiriki wa Zanzibar wanatarajiwa kuondoka kesho.
Alisema kuwa, kila mkoa utakuwa na wanamichezo 16 na hivyo msafara wa watu 80 pamoja na viongozi.
Alieleza kuwa, wanamichezo wa Zanzibar watashiriki michezo yote ikiwemo kukimbia, kurusha tufe, kisahani, mkuki na kuruka vihunzi.
Gulam alieleza matumaini yake kuwa, Zanzibar itafanya vizuri na kwamba Mkoa wa Mjini Magharibi ambao ndio mabingwa watetezi, watatetea ubingwa wao.
“Tumejipanga vizuri kushiriki michuano hii na tunatarajia kurejea na ubingwa wetu ambao Mkoa wa Mjini Magharibi iliutwaa katika mashindano ya mwaka jana”, alijigamba Katibu huyo.
No comments:
Post a Comment