Adai hawezi kulea mahaba kwa Mafunzo
Jamhuri yasema wao, Mafunzo damdam
Na Aboud Mahmoud
KOCHA Mkuu wa klabu ya Jamhuri Salum Bausi Nassor, ameamua kubwaga manyanga siku mbili baada ya kuchapwa mabao 3-2 na Mafunzo katika mchezo wa ligi kuu ya Zanzibar uliopigwa uwanja wa Amaan juzi.
Bausi amelithibitishia gazeti hili juu ya uamuzi wake huo wa kushtua, na kusema kwamba yuko huru kuondoka kwa vile hakuna mkataba aliosaini ambao unaweza kumfunga, na kwamba anakusudia kuwasilisha barua ya kujiuzulu kwake wakati wowote.
Alisema sababu kubwa inayomuondoa klabuni humo, ni kuambiwa na uongozi wakati alipowasili Pemba kuanza kazi yake, kwamba mambo yanayoihusu timu hiyo na Mafunzo awaachie viongozi.
Bausi alieleza kushangazwa na kauli hiyo, na kuongeza kuwa siri ya kuambiwa hivyo, aliibaini juzi wakati wa mechi ya ligi kuu kati ya Jamhuri na Mafunzo ambapo wageni hao kutoka Chasasa Wete, walilala kwa mabao 3-2.
Aidha, alieleza kuwa, akiwa kocha mkuu, anashangazwa na uongozi wa Jamhuri kuamua kufanya mazoezi wakati wa saa nane mchana bila yeye kupewa taarifa, huku akifahamu kuwa mazoezi yalitarajiwa kuanza saa kumi za jioni.
“Jengine ni viongozi wa timu zote hizo kwenda katika kikao cha maandalizi ya mechi (pre-match meeting), huku jezi zao zikiwa zimewekwa katika mkoba mmoja. Kwa kweli haya ni mambo ya ajabu na ndio yanayonifanya niachane na timu hiyo”, alifahamisha.
Kocha huyo mwenye msimamo wa kuwa muwazi juu ya uendeshaji soka nchini, pia alieleza kusikitishwa na hatua ya Jamhuri kufikia katika makao makuu ya klabu pinzani pamoja na kupikiwa chakula humo humo, jambo alilosema kwake ni ajabu.
Alipoulizwa juu ya hatua hiyo ya Bausi, Katibu wa Jamhuri Ahmed Omar Awadh, alikiri kuwa timu hizo mbili zina udugu wa damu uliodumu kwa miaka 30 sasa na kwamba Bausi alielezwa hilo, lakini ndani ya soka hawabebani asilani.
Hata hivyo, alieleza kuwa, wamebaini kwamba, wakati akiitwa kuifundisha timu hiyo, Bausi alitaka kila mechi wawe wanashinda, lakini akasema kwa kuwa soka ni mchezo wa ushindani, si ajabu kushindwa.
Hata hivyo, alisema huenda Bausi amepoteza hamu ya kuinoa timu yake baada ya kukataliwa kupewa mkataba wa mapema unaoambatana na malipo ya awali (advance payment), ambapo alisema Jamhuri haina utamaduni huo.
“Kama analo jengine aseme, lakini hizo sababu alizozitoa hazina msingi, sisi na Mafunzo ni ndugu wa kufa na kuzikana na hilo halitaki tochi, lakini pamoja na mapenzi yote hayo, mchezoni tunasahau udugu”, alihitimisha Awadh.
No comments:
Post a Comment