Habari za Punde

KAMISHNA WA MICHEZO ATOA ANGALIZO KWA VIONGOZI WA TIMU ZA MICHEZ

Kamishna  wa Idara ya  Michezo Zanzibar,Ameir Mohamed Makame  akizungumza na Viongozi wa Timu mbali mbali ikiwemo Timu ya Mlandege,Miembeni, Ram Sqad pamoja na  Vijana wa Uncle katika Ukumbi wa Wizara ya Habari,Vijana Utamaduni na Michezo, Migombani,Wilaya ya Mjini.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Ndugu Fatma Hamad Rajabu  amewataka viongozi wa timu mbali mbali kuhamasisha nidhamu kwa washabiki wao pamoja na kusimamia vyema viwanja vya michezo.

Akizungumza kwa Niaba, Kamishna  wa idara ya Michezo Zanzibar Ameir Mohamed Makame wakati wa kujadili mechi baina ya Timu ya Miembeni na Mlandege ambazo zinatarajia kupambana tarehe 16/05/2025 wakati wa Uzinduzi wa Uwanja wa Maisara.huko Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo,Migombani. Wilaya ya Mjini.


Alisema ni vyema kuimarisha nidhamu na maadili wakati wa michezo kwa kushangiria kwa furaha sio kutumia lugha chafu za matusi, kuvaa vijora,vinavyowadhalilisha akinamama kufanyafujo, pamoja na nyimbo za kuhamasisha matumizi ya dawa ya kulevya.


"Ondoweni migogoro tuwe na hamasa ya Michezo timu za mitaani zirudi kwenye ligi ili mechi zirudi kama zamani ndio lengo la serikali yetu kuimarisha michezo '' alisema Kamishna Ameir. 


Alieleza kuwa michezo ni chanzo cha furaha ,afya njema na kuunganisha watu wa rika na jinsia  zote ikitumika vyema huleta utulivu kuimarisha usalama na kukuza vipaji na kupelekea  kuwa  chanzo cha ajira Kwa Vijana .


aidha alifahamisha kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Husein Mwinyi ameweka miundombinu bora katika viwanja vya michezo ili kuweza kuibua vipaji kwa vijana wake hivyo iko haja ya kuvitunza ili kuwa wazalendo wa kweli kwa taifa lao.


Nae Kamishna Mkuu wa Kinga Tiba na Kurekebisha Tabia Juma Abraham Zidikheiry alisema vijana wengi wanajiingiza katika matumizi ya dawa ya kulevya kutokana na msukumo rika pamoja na migogoro ya familia jambo ambalo huchangia vijana kukosa malezi bora.


Alieleza kwamba dawa za kulevya zinazotumiwa zaidi ni bangi ikifuatiwa shisha, heroun, mirungi, cocaine pamoja na dawa tiba zenye asili ya kulevya ‘Methamphetamine’.


Alifahamisha kwamba Tatizo la Dawa za kulevya Zanzibar inakadiriwa kuwa na watumiaji  9000 ikiwa wengi wao ni Vijana kati ya  umri wa miaka 9 hadi 45, Kwa njia ya kujidunga sindano 2,735, maambukizi ya ukimwi miongoni mwa waraibu wanaojidunga ni asilimia 36, maambukizi ya homa ya ini asilimia 60 ,Kifua kikuu asilimia 11 wakati katika jamii yalikuwa ni asilimia 0.2.


Kwa upande wa Mkuu wa Intelijensia wa Madawa ya Kulevya, Haji M. Omar alisema tatizo la dawa za kulevya ni uhalifu unapangwa kwa siri kwa mitandao ya wahalifu wakubwa, wakati na wadogo au vikundi vinavyojipanga.


Alisema Dawa za kulevya ni kemikali ambazo mtu akizitumia huadhiri Mifumo wa fahamu Kwa kuleta vipumbaza ,vileta njozi pamoja na vichangamshi.


Alieleza kuwa hakuna tafiti zinazoonyesha idadi ya watu wanaotumia bangi nchini hivyo Iko haja ya kuchukuwa tahadhari na hatua za makusudi  ili kuokoa Taifa lisijeangamia .


Nae  Viongozi hao walisema  watakuwa mabalozi wazuri kwa  kufikisha ujumbe huo wa suala zima la nidhamu kwa wachezaji na washabiki wao  kiujumla ili miundombinu ya viwanja ibaki kuwa salama .  


Alisema watahakikisha wanatoa muongozo na utaratibu mzima kwa washabiki wao kuachana na nyimbo zisizostahiki kwa Jamii ikiwemo nyimbo ya Njoo Miembeni, Matusi na fujo uvaaji wa vijora pamoja na kutoa tahadhari ya kuingia viwanjani na uraibu wa aina yoyote ili kutunza mazingira yaliyopo.

Kamishna  Mkuu wa Kinga Tiba na  Kurekebisha Tabia,  Juma Abraham Zidikheiry,  Akifahamisha hali halisi ya mabadiliko ya Tabia Kwa  jamii hasa Vijana kwa kujiingiza Katika matumizi wa dawa za kulevya,(kulia) Kamishna  wa Idara ya  Michezo Zanzibar,Ameir Mohamed Makame  Katika Ukumbi wa Wizara ya Habari,Vijana Utamaduni na Michezo, Migombani,Wilaya ya Mjini
Mkuu wa Intelijensia wa Dawa za kulevya, Haji M.Omar akitoa mada kuhusu Tatizo la Dawa za kulevya  Zanzibar   katika ukumbi wa Wizara ya Habari,Vijana Utamaduni na Michezo. Migombani,Wilaya ya Mjini
Msaidizi Upelelezi wa Dawa za Kulevya Othman S.Juma akifafanua sababu zinazopelekea Vijana kujiingiza Katika uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya, Katika Ukumbi wa Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo,  Migombani,Wilaya ya Mjini .

Kiongozi wa Ram Sqad, Hafidh Othman Jabu , akielezea changamoto wanazozikabili kwa washabiki wao (wa pili kushoto  ) Mudathir Yahya Rashid pamoja na Sabra Abdallah Bakari katika  ukumbi wa Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo,  Migombani, Wilaya ya Mjini.


IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI. WHVUM.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.