Habari za Punde

Cossovo yaibomoa Maendeleo


Na Haji Nassor, Pemba
 
TIMU ya Cossovo, juzi ilimaliza majigambo yaliyokuwa yametawala kati yake na timu ya Maendeleo, kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya mahasimu wao hao wa mtaa mmoja wa Chumbageni, katika mchezo wa ligi daraja la pili Wilaya ya Mkoani kwenye uwanja wa Aston Villa..
Kwa muda wa wiki tatu zilizopita, mtanange kati ya wanaume hao uliibua gumzo kubwa, ngebe na majigambo huku kila timu ikitamba kuionesha nyengine kilichomtoa kanga manyoya.
Cossovo, ambayo mara ya mwisho ilipokutana na Maendeleo ililala kwa magoli 2-1, ilikuwa ya kwanza kuzichana nyavu za wapinzani wao kwa goli safi lililowekwa kimiani na Juma Mchunga Bakar mnamo dakika ya 20, akiunganisha pasi murua kutoka mashariki ya uwanja.
Baada ya kushtuliwa kwa goli hilo, wachezaji wa Maendeleo walikuja juu na kuhamia langoni mwa Cossovo, lakini walijikuta wakipunguzwa nguvu baada ya Juma Mchunga tena, kuongeza goli la pili katika dakika ya 30 na matokeo hayo kudumu hadi wakati wa mapumziko.
Katika kipindi cha pili, Maendeleo ilitumia vyema pengo la mshambuliaji Mohamed Bakari wa Cossovo aliyetolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi Mwalimu Hussein, kujipatia bao la kujifariji kupitia kwa Mohamed Abulrahman kwenye dakika ya 49.
Na katika mchezo mwengine uliopigwa uwanja wa Mpikatango, timu ya Aston Villa iliangukia pua kwa kuchapwa magoli 2-1 na New Scud ya Mtambile

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.