Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wazazi, Walimu na Wanafunzi mara baada ya kulizindua Jengo jipya la Madrasa hiyo
Baadhi ya Wazazi, Walimu na Wanafunzi wa Madrasatul Jamiatul Islamia ya Mto Mchanga wakiwa katika sherehe za uzinduzi wa Jengo jipya la Madrasa yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akizungumza na Uongozi wa Jumuiya wa Watu Wasioona Zanzibar { ZANAB } uliofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kumsalimia.
Wa mwanzo ni Bibi Zainab Abdulla Mshika Fedha wa Jumuiya hiyo, kati kati Bwana Adil Mohd Ali Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo na wa mwisho ni Bwana Mohd Kassim Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo
Na Othman Khamis Ame
Misingi imara itakayobuniwa na kupangwa na wazazi kwa kushirikiana na Walimu katika kuwapatia Taaluma sahihi ya Dini Watoto wao kupitia Kitabu Kitakatifu cha Quran ndio njia pekee itakayozalisha Jamii iliyo bora kimaadili ndani ya Dunia ya sasa ya mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo mara baada ya kulizindua Jengo Jipya la Madrasatul Jamiatul Islamia liliopo mpakani mwa Majimbo ya Kitope na Donge hapo Mto Mchanga Wilaya ya Kaskazini “B”.
Balozi Seif alisema Wazazi, Walezi na Walimu katika Karne hii wanakabiliwa na kazi ya ziada katika kuzaa mbinu mbadala za kuwasomesha watoto wao sambamba na kuwaendeleza Vijana katika mwenendo mzuri utakaoleta faida katika Jamii.
Alisema zipo dalili za wazi zinazoonekana kwa baadhi ya Vijana kujiingiza katika vitendo viovu ikiwemo uvunjifu wa amani zinazosababishwa na upokeaji mbaya wa Tafsiri ya Quran unaofanywa kwa makusudi yanayooongozwa na baadhi ya Masheikh hapa Nchini.
Balozi Seif aliitahadharisha Jamii kujiepusha na makundi ya Watu hao yaliyoamua kwa makusudi kupotosha Watu kwa kisingizio cha cha Dini hali ambayo kama haikudhibitiwa inaweza kuibua cheche ya hatari miongoni mwa Jamii.
“ Vijana lazima msikilize Walimu wenu wanakufundisheni nini ? Kwa kufanya hivyo mtapata fursa na nguvu ya kuelewa kwa undani mambo mema yatakayokujengeeni hatma njema ya maisha yenu hapo baadaye”.Alisisitiza Balozi Seif.
Alitanabahisha kuwa Jamii imekuwa ikishuhudia vitendo vya ajabuj vinavyofanywa na baadhi ya Vijana kwa ushawishi wa Watu wachache vinavyoashiria upungufu wa maadili ya Dini na hatimae kuleta usumbufu kwa Wananchi wengine na hata Serikali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Bibi Mwanakhamis Ussi kwa fikra zake za kuanzisha Madrasa hiyo pamoja na kusifu utaratibu wa Kamati ya Madrasa kwa uamuzi wao wa kuchangia ujenzi huo kwanza kabla ya kuanza utaratibu wa maombi ya misaada kutoka kwa Wafadhili na Taasisi nyengine.
Balozi Seif alisema kitendo chao hicho cha kijasiri kimesaidia kuwajengea nguvu na uwezo wa kuendeleza ujenzi huo kwa kujiamini.
“ Tabia ya kutumia Wanafunzi kuranda na Visanduku kupita wakiomba misaada haipendezi kwani inaondoa heshima na kuleta dharau kwa Walimu na Wanafunzi husika”. Alifafanua Balozi Seif.
Katika kuunga mkono juhudi za Wazazi, Walimu na Wanafunzi hao Balozi Seif ameahidi kuchangia Kompyuta Mbili kusaidia Madrasa hiyo ili Wanafunzi wake waende na wakati wa sasa.
Katika risala yao Wazee, Walimu na Wanafunzi hao iliyosomwa na Ustaadhi Daudi Mashimba walisema licha ya kuwa kazi ya kukuza watoto katika maadili ya Kiislamu ni nzito lakini kusudia ni kukuza zaidi masomo yanayokwenda katika misingi sahihi ya Kiislamu.
Walisema katika kutekeleza azma hiyo Uongozi wa Madrasatul Jamiatul Islamia imejiandaa kuanzisha miradi ili Madrasa hiyo ifikie lengo la kujitegemea yenyewe.
Waliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na Duka la Vitabu vya Dini, Vifaa sambamba na mradi wa kushona nguo zenye maadili ya Kiislamu.
Madrasatul Jamiatul Islamia ya Mto Mchanga iliyoanzishwa miaka 20 iliyopita na Bibi Mwanakhamis Ussi ilianza na Wanafunzi Saba wakati hivi sasa tayari inasomesha zaidi ya Wanafunzi Mia Tatu.
Mapema Mwakilishi wa Jimbo la Donge ambae pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna aliwakumbusha Wazazi, Walimu na Wanafunzi hao kuendelea kushikamana katika mambo yak heir kwa lengo la kuridhiwa na Muumba.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alionana na Uongozi wa Jumiya ya Watu wasioona Zanzibar { ZANAB } Ukiongozwa na Mwenyekiti wake Bwana Mohd Kassim mazungumzo yaliyofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya ZANAB Ndugu Adil Mohd Ali alisema Uongozi wa Jumuiya hiyo pamoja na wanachama wake wameelezea faraja yao kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali Kuu katika kuwajengea mazingira bora ya miundo mbinu watu wenye ulemavu hapa Nchini.
Ndugu Adil alisema mfano hai ni mchango Maalum uliosimamiwa na Viongozi wa Juu wa Serikali wa kuchangia maendeleo ya watu wasioona na kufikia kiwango cha kuridhisha cha jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni Mia Tatu { 300,000,000/- }
Hata Hivyo Nd. Adil alizielezea baadhi ya changa moto zinazowakabili watu wasioona kuwa ni pamoja na ukosefu wa fungu maalum la fedha kwa ajili ya maktaba ya wanafunzi wasioona wanaoingia vyuo Vikuu.
Changamoto nyengine alizitaja kuwa ni ufinyu wa Walimu wenye uwezo kamili wa kusomesha watoto wasioona, kigugumizi cha kanuni za watu wenye ulemavu, ubovu wa Bara bara iendayo kwenye Makao Makuu ya Ofisi yao pamoja na kupata Baraka za Baraza la wawakilishi kwa azimio la Umoja wa Mataifa linaloelezea sheria za Kimataifa za kulinda haki za watu wenye ulemavu { UNCRPD } ambalo tayari limesharidhiwa na Bunge la Muungano.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuhakikishia Uongozi wa Jumuiya ya Watu wasioona Zanzibar { ZANAB } kwamba Serikali itaendelea kujenga miundo mbinu itakayowawezesha watu wenye ulemavu kupata huduma sawa na watu wengine katika Ofisi na Taasisi zote za Umma.
Balozi Seif alisema Binaadamu lazima waendelee kupendana na kuheshimiana, na katika kutimiza hilo haki na thamani ya watu wenye ulemavu inafaa kuzingatiwa ipasavyo katika Jamii.
Katika kuunga mkono harakati za Jumuiya hiyo ya watu wasioona Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliahidi kumaliza ahadi yake aliyoitoa ya shilingi 1,000,000/- katika kuchangia Maendeleo ya Jumuiya hiyo inayotarajiwa kufanya Mkutano wake Mkuu wa Mwaka kuanzia Tarehe 6 hadi 8 Disemba mwaka huu.
Pia Balozi Seif aliahidi kuangalia uwezekano wa kusaidia Vijana wa Jumuiya hiyo walioamua kushiriki katika mazoezi ya mchezo wa Shall Down uliofanana na Table Tennis kwa kuchangia matengenezo ya sehemu Maalum ya Mchezo huo hapo Makao Makuu ya Ofisi yao iliyopo Kikwajuni.
No comments:
Post a Comment