Habari za Punde

Burundi hawatunyimi usingizi - Cannavaro

Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
 
NAHODHA wa Zanzibar, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ amesema kwamba hawawahofii hata kidogo Burundi japokuwa hawajafungwa hata mechi moja kwa sasa katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge, yanayoendelea mjini hapa.
 
Zanzibar Heroes, ambayo haina wadhamini, itapambana na Burundi kesho katika Robo Fainali kwenye Uwanja wa Lugogo mjini hapa, mchezo ambao utatanguliwa Robo Fainali nyingine kati ya Tanzania Bara na Rwanda.
 
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini hapa, beki huyo wa Yanga SC ya Dar es Salaam, alisema kwamba anakubali Burundi ni timu nzuri, lakini watapigana kiume kuhakikisha wanashinda na kuingia Fainali.
 
“Sisi tumekuja hapa kuchukua Kombe, kwa hivyo hatuhofii timu yoyote, ndiyo Burundi wazuri, wameifunga Bara, lakini sisi ni Zanzibar, na tutapambana kiume tuwatoe,”alisema Cannavaro.
 
Akiuzungumzia mchezo wa jana ambao walifungwa 2-0 na Malawi, Cannavaro alisema kwamba hawakutaka kutumia nguvu nyingi kwa sababu walikuwa wana uhakika wamekwishafuzu.
Sisi baada ya kuona kwamba tunaongoza Kundi kabla ya mechi za mwisho na kupiga hesabu zetu vizuri baada ya matokeo ya mwisho, tutafuzu tu, tukaamua tusitumie nguvu nyingi, ili zije kutusaidia katika Robo Fainali,”alisema Cannavaro.
 
Na Bin Zubeiry kutoka Kampala

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.