Watoto na vijana mbali mbali wa Wilaya ya Kilindi Tanga wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Wilayani humo.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Handeni sokoni Mkoani Tanga.
Wananchi mbali mbali wa Wilaya ya Handeni Tanga wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Handeni sokoni. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Na Hassan Hamad, Handeni Tanga
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema sekta za elimu na kilimo bado hazijapewa umuhimu unaostahiki katika kumkomboa Mtanzania kiuchumi.
Amesema elimu inayotolewa hasa katika skuli za vijijini bado ni duni, na kwamba skuli hizo zimekuwa zikikabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu pamoja na vifaa vya kufundishia.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya za Kilindi na Handeni Mkoani Tanga katika mikutano ya hadhara iliyoandaliwa na Chama hicho kwa nyakati tofauti, Maalim Seif amesema wananchi hao wa vijijini pia wamekuwa wakisumbuliwa na ada kubwa ya skuli kulinganisha na uwezo wa kipato chao.
Ameishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuangalia uwezekano wa kuzisaidia skuli hizo kwa kuzipatia walimu na vifaa vya kufundishia, ili wanafunzi hao wapate elimu sawa na wale walioko maeneo mijini.
Akizungumzia kuhusu kilimo, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na bajeti ndogo ya kuendeleza sekta hiyo.
Amezitaja changamoto nyengine kuwa ni pamoja na elimu duni ya kilimo kwa wakulima, bei kubwa za pembejeo za kilimo pamoja na ukosefu wa soko kwa bidhaa mbali mbali zinazozalishwa na wakulima wazalendo.
Amesema iwapo serikali itaweka mkazo katika sekta hiyo na kuwawezesha wakulima kumudu gharama za uzalishaji, wananchi wengi wataweza kujikomboa kutokana na kilimo ambacho kitawaletea tija.
Amesema Zanzibar kupitia serikali ya umoja wa kitaifa imeshaanza kuona umuhimu wa kuwawezesha wakulima, baada ya kuamua kupunguza bei ya pembejeo za kilimo na gharama za kulimia, na kwamba sasa mahitaji ya pembejeo za kilimo yamekuwa makubwa kwa vile wananchi wengi wanaweza kumudu gharama hizo, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Amefahamisha kuwa iwapo chama hicho kitapata ridhaa ya kuongoza nchi kitaweka mkazo zaidi katika sekta za elimu na kilimo ili kuleta ukombozi wa kweli wa kiuchumi kwa Watanzania.
Mapema akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni bw. Muhingo Rweyemamu, ameeleza hatua ya Zanzibar kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa kuwa ni yenye mafanikio na ya kupongezwa duniani kote.
Amesema faida za kuwepo kwa mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar ni nyingi ikilinganishwa na hasara zake, na kwamba hatua hiyo imeonesha ukomavu wa kisiasa na kukuwa kwa demokrasia visiwani Zanzibar.
Wakati huo huo Chama Cha Alliance for Democratic Change ADC kimepata pigo jengine baada ya wanachama wake (120) wakiongozwa na katibu wa vijana wa Chama hicho Wilayani Handeni Rajab Abdallah Shiza kujiengua na kujiunga na CUF.
Akizungumza katika mkutano huo bwana Shiza amesema wamefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa ndani ya Chama hicho kuna ubabaishaji ikiwa ni pamoja na kuwadanganya na kuwatapeli wananchi wa maeneo mbali mbali.
“Walikuja hapa viongozi wetu wa ADC wakatuambia kuwa watatupatia mikopo ili tuweze kuendesha miradi mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikundi vya ushirika, lakini hadi leo baada ya kupata usajili hatujaona mkopo wala taarifa yoyote inayohusiana na mikopo” alifahamisha Shiza.
Katika mikutano mitatu tofauti aliyofanya Mkoani Tanga, Maalim Seif aliwasisitiza wananchi kupima sera za vyama, ili kufanya maamuzi sahihi wakati wanapochagua viongozi wa kuwaongoza.
No comments:
Post a Comment