Habari za Punde

Tume ya uchaguzi inayomaliza muda wake yakabidhi ripoti yake kwa Makamu wa kwanza wa Rais

  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC waliofika nyumbani kwake Mbweni kwa ajili ya kumkabidhi ripoti ya ZEC ya miaka mitano pamoja na kukuaga baada ya kumaliza muda wao wa utumishi katika tume hiyo. Pamoja nae ni Mwenyekiti wa tume hiyo Khatib Mwinyichande
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akipokea ripoti ya miaka mitano ya ZEC kutoka kwa Mwenyekiti wa tume hiyo Khatib Mwinyichande
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC waliofika nyumbani kwake Mbweni. Waliokaa ni Mwenyekiti wa tume hiyo Khatib Mwinyichande ( koshoto) na Makamu mwenyekiti Said Bakar Jecha.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiagana na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC Salum Kassim Ali baada ya mazungumzo na wajumbe wa tume hiyo yaliyofanyika nyumbani kwake Mbweni. Kushoto ni Mwenyekiti wa tume hiyo Khatib Mwinyichande. (Picha na Salmin Said,OMKR)

Na Hassan Hamad, OMKR
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Sharif ameelezea matarajio yake kuwa tume mpya ya uchaguzi itakayoundwa Zanzibar itafanya kazi kwa kujiamini zaidi ili kukidhi matakwa ya wananchi.
 
Amesema iwapo Tume ya uchaguzi itafanya kazi kwa kujiamini na kuacha kufuata matakwa ya wanasiasa, itajenga imani kwa wananchi juu ya uwezekano wa kuwepo kwa chaguzi huru na za haki.
 
Maalim Seif ameeleza hayo leo nyumbani kwake Mbweni Zanzibar, wakati akizungumza na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC waliofika kwa ajili ya kumkabidhi ripoti ya utendaji wa tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitano, pamoja na kumuaga baada ya kumaliza muda wao wa utumishi ndani ya tume hiyo.


Amesema kazi iliyofanywa na tume hiyo ni nzuri, lakini tume inayokuja inapaswa kujifunza kutokana na tume hiyo ili kufanya kazi zake kwa kufuata misingi ya sheria na kuongeza ufanisi wa Tume.
 
Ameelezea haja kwa tume hiyo kuanzisha mfuko wake, ili mapato ya tume yaingie moja kwa moja katika mfuko huo na kupunguza usumbufu wakati tume inapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi yake ya kawaida.
 
Hata hivyo Maalim Seif amesema tume hiyo inayomaliza muda wake mwishoni mwa mwezi huu, inaondoka huku ikiwacha viporo ambavyo tume inayokuja inapaswa kuvipa umuhimu wa kipekee.
 
Miongoni mwa mambo ambayo hayakuweza kutekelezwa na tume hiyo ni pamoja na kushindwa kulifanyia uhakiki daftari la kudumu la wapiga kura kwa vipindi viwili tofauti, jambo ambalo liliahidiwa na tume hiyo kufanyika kila ifikapo mwezi wa Oktoba.
 
Kamishna wa Tume hiyo bw. Ayoub Bakar Hamad amesema tatizo hilo lilitokana na ukosefu wa fedha za kuendeshea kazi hiyo, na kwamba kwa sasa Shirika la Umoja wa Mataifa la UNDP tayari limekubali kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza kazi hiyo.
 
Amesema iwapo fedha hizo zitapatikana kwa wakati mapema mwezi ujao, tume ijayo itakuwa na uwezo wa kufanya uhakiki mara mbili kwa mwaka, ili kufidia muda uliopita.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume hiyo Bw. Khatib Mwinyichande amesema jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa katika kuimarisha demokrasia ya uchaguzi Zanzibar.
 
Amesema Tume inayokuja inaweza kufanya kazi zake vizuri zaidi iwapo wanasiasa watatoa ushirikiano wa kutosha kwa tume hiyo sambamba na kukubali kufuata sheria zilizowekwa.
 
“Naomba wanasiasa musioneane haya, shaurianeni na kubalini kukosoana, na kubwa zaidi ni kukubali kufuata sheria”, alishauri Mwinyichande na kuongeza,
 
“Wanasiasa pia munayo nafasi kubwa ya kuisaidia tume kwa kuipa maelekezo yanayostahiki, na kufanya hivyo kunaweza kuipa nyenzo bora za kufanyika kazi”, aliongeza.
 
Nae mkurugenzi wa Tume hiyo Bw. Salum Kassim Ali, ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika chaguzi zilizopita, ili kuweka mazingira bora zaidi katika chaguzi zijazo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.