Habari za Punde

Zantel yatoa msaada wa dawa hospitali ya Mafia

 Bwana Ibrahim Attas, Meneja Masoko wa Zantel, akikabidhi msaada wa madawa kwa Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya ya Mafia-Anael Pallangy, pamoja na kaimu Matron, Rukia Maungo.

Meneja Masoko wa Zantel-Zanzibar, Ibrahim Attas, akikabidhi maji ya kunywa na soda, pamoja na msaada wa madawa kwa Mganga mkuu wa Hospitali ya Mafia, Anael Pallangy, pamoja na kaimu matroni wa Hospitali hiyo, Rukia Maungo.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Bwana Mohamed Kimbau (Wa pili kushoto ) akiwa na msaada wa madawa aliokabidhiwa na kampuni ya simu ya mikononi ya Zantel. Kutoka kushoto ni Meneja Masoko wa Zantel, Ibrahim Attas,Mganga mkuu wa Hospitali ya Mafia, Anael Pallangy (kulia) akifuatiwa na Katibu tawala wa wilaya hiyo, Mr Usasi.

Kampuni ya simu za mikononi ya Zantel imetoa msaada wa dawa zenye thamani ya milioni 5 kwa hospitali ya wilaya ya Mafia ikiwa ni juhudi za kampuni hiyo katika kusaidia kuboresha huduma za afya wilayani humo.
 
Msaada huo muhimu sana katika hospitali hiyo, ambayo pamoja na ukosefu wa madawa, bado inakabiliana na changamoto kadhaa kama uchache wa wahudumu wa afya, unatarajiwa kusaidia zaidi ya wagonjwa 1000 hospitalini hapo.
 
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Afsa biashara wa Zantel-Zanzibar, bwana Mohamed Mussa alisema kampuni yake inatoa umuhimu mkubwa na wa pekee katika maeneo inayofanyia biashara.

‘Kampuni yetu ina furaha sana katika kusaidia jamii yetu kuboresha huduma za afya, kwani bila jamii yenye afya bora biashara yetu haiwezi kukua’ alisema Mussa.
 
Akizungumzia zaidi msaada huo, bwana Mussa anasema Zantel imejikita katika kuhakikisha jamii za pembezoni zinapata huduma bora za afya kwani mara nyingi zimekua zinasahaulika sana.
 
Akipokea msaada huo, Mkuu wa wilaya ya Mafia, Mheshimiwa Sauda Mtondoo aliipongeza kampuni ya Zantel kwa msaada huo akisema umekuja kwa wakati muafaka kwani hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa madawa hasa kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa.
 
‘Tunaishukuru kampuni ya Zantel kwa kuchagua kusaidia hospitali yetu, na naziomba kampuni nyingine ziige mfano huu, hasa kwa kusaidia hospitali za pembezoni kama yetu ambazo zimesahaulika sana’ alisema mheshimiwa Mtondoo.
 
Hospitali ya wilaya ya Mafia ina wodi 6 ikiwa na jumla ya vitanda 84 na kwa sasa inahudumia wagonjwa 100 kwa siku, ikiwa ni hospitali tegemezi willayani humo.

1 comment:

  1. Haya ndiyo mambo tunayotarajia kuyaona kutoka Z'ntel.

    Lzma wakubali ukweli kua undugu uliopo kati yetu na wenzetu wa Mafya ndio uliowafanya waipokee Z'tel kwa mikono miwili hivyo kuwakumbika ni wajibu!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.