Habari za Punde

Dk. Shein ahudhuria Taarabu rasmi ya miaka 49 ya Mapinduzi

Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mwanamwrema Shein,akitunza katika Taarab rasmi iliyocharazwa na Kikundi cha Taifa cha Zanzibar, katika kusherehekea Maadhimisho ya Miaka  49 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,huko katika
ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,(wa pili kulia)akiwa Mgeni Rasmi katika Taarab ya Kusherehekea Miaka 49 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar iliyopigwa na kikundi cha Taifa,katika ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Zanzibar
jana,(kulia) Naibu Waziri wa Habari,Utalii,Utamaduni na Michezo Bihindi Hamadi Khamis,Mke wa Rais Mama Mwanamwema Shein,(kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdalla Mwinyi Khamis,(wa pilikushoto),pamoja na wananchi wengine
 
Na Rajab Mkasaba, Ikulu
 
KIKUNDI cha Taifa cha Taarab cha Zanzibar jana usiku kilitia fora kwa kutoa burdani ya aina yake ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za sherehe za kutimiza miaka 49.; ya Mapinduzi ya Zanzibar, kutokana na nyimbo zake zilizoisisimua hadhira.
Taarabu hiyo rasmin ilifanyika katika ukumbi wa Salama Bwawani, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein akiwa pamoja na Mama Mwanamwema Shein na viongozi wengine mbali mbali wa vyama na serikali pamoja na wageni waalikwa kutoka ndani na nje ya Zanzibar.
Nyimbo mbali mbali ziliimbwa na waimbaji mahiri na wenye sauti za kumtoa nyoka pangoni kutoka katika kikundi hicho ambacho kinaundwa na waimbaji pamoja na wapigaji wa muziki kutoka Unguja na Pemba hali ambayo iliwafanya baadhi ya wageni waalikwa waliohudhuria washindwe kukaa vitini mwao.
‘Rais Tunakupenda’ ndiyo nyimbo iliyofungua dimba katika hafla hiyo iliyoimbwa na Ma-Al-Anisa wawili akianza Asha Ali kutoka Pemba na kufuatiwa na Sihaba Juma kutoka Unguja, wimbo uliompongeza Dk. Shein kwa juhudi zake katika kusimamia Utawala Bora pamoja na mikakati yake ya kuendeleza kilimo hasa kile cha kisasa ikiwa ni pamoja na kuongeza bei ya zao la karafuu.
Nyimbo hiyo pia, ilimsifu na kumpongeza Dk. Shein kwa kuendelea kusimamia vyema amani na utulivu iliyopo nchini ambayo ndio muhimili mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
“Ni arubaini na kenda myaka tuliyofikiya, Rais tunakupenda kwa unavyotufanyia, Hakuna linalokushinda sote watutumikiya”, ni kiitikio ya nyimbo hiyo ambayo pia ilisifu nasaha na wito aliokuwa akitoa Dk. Shein wa kutoa maoni juu ya Katiba mpya sanjari na kutovunja sheria zilizowekwa.
Sifa juu ya kuondoa kero kwa wazazi kutolia wakati wa kujifungua ni miongoni mwa mashairi yaliopamba nyimbo hiyo.
Kila nyimbo iliyoimbwa katika hafla hiyo ilitia fora ambapo miongoni mwa nyimbo hizo ni kama ile ‘Siri ya Moyoni’, iliyoimbwa na Al- Anisa Fauzia Abdalla, ’Sema’, iliyoimbwa na Fatma Issa, na nyenginezo.
Makame Faki au kwa jina la usanii ‘sauti ya zege’ hakuwa nyuma kwani aliweza kuiteka hadhira na kuwafanya baadhi ya wageni waalikwa washindwe kukaa katika viti vyao kutokana na mahadhi na ujumbe wa nyimbo hiyo pamoja na vinanda vyake vilivyoenda sambamba nyimbo ambayo mbali ya kuiimba pia ameitia muziki.
Wakongwe wa taarabu asilia Al-Anisa Saada Mohammed na nyimbo yake ‘Chaguo’ nayo ilitumbuiza vizuri kutokana na ujuzi na utaalamu wa uwimbaji wa nyimbo hiyo huku watu wengi ukiwakumbusha enzi hizo na kuonekana kuwa dhahabu haiozi.
Al-Anisa Mtumwa Mbarouk naye hakuwachwa nyuma katika kutoa burudani ya taarabu asilia na kuweza kuburudisha hadhira na nyimbo yake ya ‘Mpewa Hapokonyeki’.
Mkurugenzi wa Kikundi hicho Iddi Suwedi nae alionesha umahiri wake kati fani hiyo baada ya kuimba nyimbo yake ya ‘ Kinacho wasumbueni’ iliyotungwa na Mohammed Ahmed na kutiwa muziki na mwenye Mkurugenzi Idd.
Hilda Mohammed na wimbo wake ‘Nnavyokupenda’ aliutunga na kutia muziki Bi Fatma Issa na yeye mwenyewe ndio alioutunga.
Nyimbo ya ‘Hakika Nnakupenda’ iliyoimbwa na Muimbaji Ali Masoud ambayo asili yake nyimbo hii iliimbwa na Al-Marhum Seif Salum ambaye yeye mwenyewe aliitunga, ilikonga sana nyoyo za watu waliohudhuria hafla hiyo.
Taarabu hiyo rasmin ni miongoni mwa sherehe za kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ambapo miongoni mwa viongozi waliohudhuria katika ni pamoja na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Abdalla Mwinyi Khamis wake wa Makamu wa Pili wa Rais Mama Asha Idd na Mama Pili Idd, Mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mama Zakia Bila.
Wengine ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Utalii na Michezo Mhe. Bi Hindi Hamad Khamis , Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Jihadi Hassan, Naibu Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Perera Ame Silima pamoja na viongozi wengine wa vyama na serikali na wananchi kutoka sehemu mbali mbali.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.