Na
Hafsa Golo
MARADHI
ya homa ya mapafu yanaendelea kuathiri katika kijiji cha Matemwe na kusababisha
zaidi ya mbuzi 150 kufariki.
Wananchi
wamepata hofu kuwa maradhi hayo huenda yakasambaa kwa binadamu kwa kuwa wamekuwa
wakila nyama za mbuzi waliokufa kutokana na ugonjwa huo.
Kwa
mujibu wa taarifa zilizotolewa na Daktari wa Mifugo Matemwe, Silima Mtwana
Khamis maradhi hayo yamekuwa tishio kubwa kwa mbuzi, ambapo kati ya mbuzi 10
hadi 20 hufa kwa siku.
Alisema
maradhi hayo yameingia katika kijiji hicho yakitokea Mkoani Tanga kutokana na
ukiukwaji wa taratibu za kusafirisha wanyama.
"Wafugaji
wana tabia ya kuingiza wanyama kwa njia za panya na kuacha kufuata taratibu
hivyo wanyama huingia bila ya kuangaliwa na wahusika wa afya na maradhi haya
yametokea Tanga,” alisema.
Aliiomba
serikali kupeleka huduma za afya kwa wanyama ili kuepusha tatizo hilo kusambaa kwa mifugo
mingine ikiwemo ng’ombe.
Aidha
aliwataka wananchi kuwa na tahadhari wanapokula nyama ya mbuzi aliyefariki
kutokana na ugonjwa huo.
Mfugaji
wa mbuzi Mawazo Silima Mawazo, mkaazi wa Mbupurini Matemwe aliiomba serikali
kuwapatia madaktari wa mifugo ili kuwapatia chanjo wanyama wao pamoja na kuwaelimisha wafugaji njia sahihi za kujikinga na ugonjwa huo.
Naye
Mohamed Hamrani Khamis, mkaazi wa Tundanga alisema maradhi hayo yamekuwa
yakienea kwa kasi katika vitongoji mbali mbali vya Matemwe, ambapo kwa siku
zaidi ya mbuzi 50 hufa au kuchinjwa baada ya kuonekana kuwa na dalili za
ugonjwa huo.
Tayari
mbuzi 345 wameshapatiwa matibabu tokea ugonjwa huo uibuke.
No comments:
Post a Comment