Na Ali Issa Maelezo-Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewasilisha Waraka wa Mapendekezo ya marekebisho ya sheria namba 6 ya mwaka 1997ya kuvipatia Ruzuku Vyama vya Siasa vitakavyo shinda katika chaguzi na kuingia madarakani ili kuondoa kasoro zilizopo katika sheria hiyo.
Akiwasilisha Waraka huo leo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed amesema malengo makubwa ya sheria hiyo ni kuiwezesha Serikali kutimiza wajibu wake wa kuimarisha demokrasia na utawala bora kwa kuvipatia ruzuku vyama vilivyotimiza masharti ya kupewa ruzuku hiyo ili vijiendeshe vizuri.
Kwa mujibu wa sheria hiyo Vyama vitakavyopata ruzuku hiyo ni vile vilivyoshinda kiti cha Urais, viti vya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Viti vya Madiwani katika chaguzi zinazofanyika nchini.
Amesema sheria ya ruzuku ilipitishwa mwaka 1997 kwa madhuumuni makubwa ya kuwezesha Serikali kutimiza wajibu wake kwa misingi ya kuimarisaha demokrasia na utawala bora nchini kutokana na nafasi ya vyama vya siasa kuwa ni nguzo kuu ya demokrasia na muelekeo wa Taifa.
Amesema tokea kupitishwa kwa sheria ya ruzuku kwa vyama vya siasa, utekelezwaji wake ulishindikana kutokana na sheria hiyo kueleza kuwa Ruzuku itakayotolewa na Serikali isipungue asilimia moja ya bajeti ya kawaida ya kila mwaka kiwango ambacho ni kikubwa sana hasa ikizingatiwa changamoto za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Jambo jingine lililopelekea malalamiko ni Sheria hiyo kueleza kuwa mgawanyo wa Ruzuku ya asilimia 50 ya Ruzuku kipewe chama kilichopata kiti cha Urais,asilimia 30 zinagaiwa kwa mujibu wa uwiano wa viti vya majimbo ya wawakilishi, na asilimia ishirini 20 kwa mujibu wa uwiano wa viti vya wadi.
Waziri Aboud alisema mgawanyo huo umekua ukilalamikiwa sana kwani hauzingatii mustakbali wa vyama vya kisiasa na uendeshaji wake bali unaleta ushindani mkubwa na mvutano katika uchaguzi wa kiti cha Urais, hivyo marekebisho hayo yanahitajika ili kuiwezesha sheria hiyo kutekelezeka kwa manufaa yaliokusudiwa.
Waziri Aboud amesema baada ya majadiliano hayo ya marekebisho amependekeza kifungu cha tatu cha sheria hiyo kita kuwa kima cha chini kitakacho tolewa na serikali kisizidi asilimia moja ya bajeti ya kawaida ya kila mwaka ya serikali .
Amefahamisha kuwa kifungu cha tano cha sheria hiyo kifanyiwe marekebisho kwa kuweka mgawanyo mpya wa Ruzuku ambapo asilimia 20 ya ruzuku iende kwa chama kilicho shinda kiti cha Urais ,asilimia 50 ya ruzuku itagaiwa kwa uwiano wa viti vya majimbo ya uwakilishi na asilimia 30 ya Ruzuku itagaiwa kwa uwiano wa viti vya udiwani katika wadi.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Baraza la Waawalikshi ya kusimamia Ofisi za viongozi wakuu wa kitaifa Mwanajuma Faki Mdachi wakati alipokuwa akitoa Mapendekezo ya kamati hiyo aliiomba Serikali iweke asilimia maalum ya ruzuku kwa vyama vya siasa ambavyo havikuingia madarakani vilivyo shiriki uchaguzi kwa kuangalia kura zao ili kuweza kuimarisha demokrasia na uhai wa vyama hivyo.
Aidha alishauri kuwa vyama vya siasa ambavyo havina viti vya Uwakilishi na Udiwani Zanzibar viungane ili viweze kuongeza nguvu ya kushinda katika chaguzi mbalimbali.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment