Habari za Punde

Dk. Shein abainisha umuhimu Vitambulisho vya Taifa · Asema ZanID kuendelea kutumia


Na Mwashamba Juma
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza umhimu wa Tanzania kuwa na vitambulisho vya Taifa kwa kufafanua mambo kadhaa muhimu yatayopatikana kutokana na vitambulisho hivyo.

Alisema vitambulisho vya taifa vitaisaidia serikali katika utendaji wake ikiwemo kufanikisha juhudi zake za kudhibiti wafanyakazi hewa.

Aidha alisema vitasaidia kuimarisha usalama pamoja na kurahisisha kupeleka huduma za kijamii  kwa wananchi ikiwemo miundombinu.

Dk. Shein aliyasema hayo jana viwanja vya Baraza la Wawakilishi Chukwani katika sherehe za utoaji wa vitambulisho vya taifa awamu ya kwanza kwa Zanzibar.

Alisema vitambulisho vya taifa pia vitawarahisishia wananchi kupata huduma muhimu zikiwemo mikopo kutoka taasisi za kifedha, wanafunzi kupata mikopo kwa ajili ya masomo, sambamba na kuzirahisishia  taasisi hizo kupata wepesi wa kurejeshewa fedha zao kutoka kwa wakopaji.


Aliwataka wananchi kuitumia fursa hiyo kwa kuandaa nyaraka zao muhimu zitakazotoa taarifa sahihi na kuachana na kasumba za wasioipendelea mema nchi kwa kulichukulia suala la vitambulisho kuwa ni la kisiasa.

Aidha amewataka wafanyakazi wa NIDA kuweka mbele maslahi ya nchi wakati wa utoaji wa vitambulisho hivyo kwa kuhakikisha mtu asiestahiki hapatiwi kitambulisho hicho.

Akizungumzia suala la vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi, Dk. Shein alisema vitaendelea kutumika kama kawaida kwa mahitaji yote kama ilivyopangwa.

Hata hivyo, alizitaka mamlaka husika kuwa na ushirikiano wa hali ya juu ili kukamilisha zoezi la utoaji wa vitambulisho vya taifa kama ilivyokusudiwa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima alisema mfumo wa ugawaji vitambulisho vya taifa utaisaidia serikali kuwa taarifa sahihi za wananchi wake, wageni ,wakimbizi mahalali wanamoishi na kazi wanazofanya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambusho vya Taifa, Dickson Maimu alisema lengo la kuanzishwa vitambulisho ni kutambua raia halali wa Tanzania pamoja na wageni wanaoishi nchini.

Mkurugenzi huyo alisema licha ya mradi kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo fedha kwa ajili ya uendeshaji lakini walifanikiwa kutoa vitambulisho hivyo kwa awamu ya kwanza Februari 7 mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo Rais  Jakaya Kikwete alikuwa Mtanzania wa kwanza kupatiwa kitambulisho hicho.

Aliongeza kuwa changamoto nyengine ni wananchi kutokuwa na baadhi ya taarifa sahihi ikiwemo kukosa viambatanisho muhimu vitakavyoweza kumtambulisha kwa urahisi.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alizitaka kamati za ulinzi na usalama ngazi ya shehia na mitaa, Idara ya Uhamiaji,jeshi la polisi na usalama wa taifa kuwa na mashirikiano ya karibu kuhakikisha waombaji wasiokuwa raia Watanzania wanaenguliwa.
 Katika hafla hiyo, Dk. Shein alikabidhiwa kitambulisho chake na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani.

Baadae Dk. Shein alikabidhi vitambulisho hivyo kwa viongozi mbali mbali akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, Mwanasheria Mkuu, Othman Masoud, wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama Zanzibar, pamoja na Mkuu wa majeshi ya ulinzi, Davis Mwamunyange.

Wengine ni Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, Mawaziri wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Makatibu wakuu na watendaji wengine wa serikali, pamoja na wawakilishi wa vyama vya siasa na wananchi wa Pemba na Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.