Habari za Punde

Jukwaa la Katiba lataka Madiwani wasiwe wajumbe mabaraza ya katiba mpya



Na Fatuma Kitima,DSM

JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKITA) limesema katika muongozo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba juu ya muundo na utaratibu wa kupata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya na asasi una mapungufu katika baadhi  ya vipengele.

Akizungumza Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba alitaja baadhi ya mapungufu hayo kuwa Madiwani wasiwe wajumbe wa moja kwa moja wa mabaraza ya katiba ya Wilaya,maoni  juu ya mwongozo yametolewa na watu wachache,sifa za watakaochaguliwa kuwa wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya pia zina mapungufu.

Deus alisema ili kupanua wigo wa demokrasia na kuepuka mgongano wa kimaslahi, Jukwaa limependekeza kuwa Madiwani wasiei wajumbe wa moja kwa moja kwa nyadhifa zao,katika mabaraza ya Wilaya ,ngazi ya serikali za mitaa na badala yake wanaotaka kuwa wajumbe waombe ridhaa  mpya ya wananchi ili kuweza kuchaguliwa katika mabaraza hayo.

Alisema sababu za kutoa mapendekezo hayo kuwa Madiwani wasingie kwa nafasi zao kwa sababu Madiwani walichaguliwa kwa ajili ya kazi ya kuwawakilisha wananchi katika ngazi ya mabaraza ya Madiwani ya Wilaya,manispaa,miji na majiji na si kwa ajili ya mabaraza ya katiba.


Alieleza wawakilishi wanne watakaochaguliwa kutoka kila kijiji na kata watakuwa na mamlaka stahili ya kuwakilisha wananchi kama ilivyo kwa Madiwani katika mabaraza ya Madiwani.

Alifafanua kuwa uwakilishi wa Madiwani utaleta mgongano wa itikadi za vyama vilivyowaweka Madiwani hao madarakani hivyo kuleta msuguano kwenye mchakato wa mabaraza ya katiba.

Aidha alisema kuingia kwao moja kwa moja kutaweka mazoea mabaya kwa vyombo vitavyoundwa siku za baadae katika mchakato huo wa katiba pamoja na kuleta utata juu  ya endapo Wabunge ambao nao ni wajumbe kwa nyadhifa zao.

Sababu nyingine kuwa Madiwani jukumu lao ni usimamamizi wa shughuli za maendeleo na masuala ya uongozi na siasa katika kila kata hivyo wanashauriwa Madiwani wabaki hivyo ili wasaidie wanapohitajika katika majukumu hayo ya kila siku kuliko wakiwa wajumbe katika mabaraza ya katiba.

Alisema walibaini kuwa muongozo unatoa madaraka yasiyo na ukomo kwa watendaji wa vijiji na masheha katika kuratibu zoezi la upatikanaji wa wajumbe wa mabaraza ya katiba.

Alisema Pamoja na mapendekezo hayo, muongozo utamke bayana namna madaraka hayo yanavyodhibitiwa kwa kutamka watu wanaoweza kumzuia asiweke upendeleo kwa baadhi ya watu waliopendekezwa kuwa wajumbe wa mabaraza ya katiba.

Hata hivyo, alisema endapo mapungufu yatafanyiwa kazi muongozo huo utakuwa ni mfano wa kuigwa na utafanya kazi ya mabaraza ya katiba yawe ya wazi na shirikishi kwa kiwango kikubwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.