Mwantanga Ame na Gilbert Massawe
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dk. Ali Mohamed Shein, ameungana pamoja na waumini wa dini ya kikristo na
wananchi wa Zanzibar katika mazishi ya Padri Evaristus Gabriel Mushi, yaliyofanyika
Kitope mkoa wa Kaskazini Unguja.
Awali Dk. Shein, alishiriki katika ibada ya misa ya
kumuombea Padri huyo na baada alipata nafasi ya kutoa heshima zake za mwisho.
Misa hiyo ilifanyika katika kanisa la Minara miwili mjini
Unguja, ambapo Kadinali Policarp Pengo aliongoza misa ya kumuombea Padri huyo.
Maziko hayo yalihudhuriwa na umati mkubwa wa waumini wa
kikiristu na wananchi wa Zanzibar ambao waliguswa kwa karibu na kifo cha Padri
huyo.
Vilio, simanzi na huzuni vilitawala katika mazishi hayo
huku kukiwa na misururu mikubwa ya
magari na ulinzi ukiimarishwa kila kona.
Akitoa salamu zake kwa wananchi, viongozi wa dini wa
kikristo na aaumini wa makanisa, Dk. Shein alisema serikali imepokea kwa
mshtuko mkubwa kifo cha Pardi Mushi na itahakikisha wahusika wanakamatwa popote
walipo.
Katika salamu zake zilitolewa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, Dk. Shein alisema kifo
hicho hakijaacha pengo kwa familia yake bali kimeigusa sehemu kubwa ya jamii ya
Watanzania na haiwezkani serikali kukaa kimnya kunyamazia uovu huo.
Alisema tayari serikali imeanza kufanya uchunguzi wa
matukio yaliojitokeza na itahakikisha inakomesha matukio ya aina hiyo.
Alisema Padri Mushi alipenda kuhubiri mambo mema yenye kusimamia haki na kulinda heshima katika jamii na kuondoka kwake kumeiumiza jamii.
Dk. Shein, alishiriki mazishi hayo akiwa pamoja na
viongozi mbali mbali wa serikali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif
Sharif Hamad, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Katibu Mkuu wa Chama
cha CHADEMA, Wilbroad Slaa na Mwenyekiti
wa NCCR Mageuzi, James Mbatia.
Nae Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Mrisho Kikwete,
akitoa salamu zake ambazo ziliwakilishwa na mmoja wa watendaji wa kanisa hilo,
alisema serikali imepokea kwa masikitiko makubwa kifo hicho na imewataka
waumini wote wa dini ya kikristo kuendelea kuishi kwa amani na upendo.
Alisema serikali itahakikisha kuwa hatua stahiki
zinachukuliwa kwa wahusika kwani itafanya upelelezi wa hali ya juu ili kuukata
mzizi wa fitina wa matukio hayo.
Mmoja wanafamilia akitoa salamu kwa niaba ya familia,
alisema msiba huo umeiumiza kwa kiasi kikubwa familia yao kwa vile Pardi Mushi
hakufa kwa kuugua bali amedhulimiwa kwa kukatishwa maisha yake.
Alisema familia inaushukuru uongozi wa kanisa, serikali
na daktari aliyemfanyia uchunguzi mwili wake na kusema wana matumaini makubwa
kuweza kupata majibu mazuri ya uchunguzi unaofanywa.
Akitoa hotuba maalum katika misa ya sala ya kumuombea marehem,
Rais wa Baraza la Maskofu Makanisa Katoliki Tanzania, Askofu, Tarikisius
Ngalalekumtwa, alisema thamani ya maisha ya binadamu ni kuishi kwa upendo na
haki.
Alisema kifo cha Padri Mushi, kisichukuliwe kama ni
maadhimisho ya kifo ila watambue namna ya kujenga uhai kwa kuacha maovu kwa
kutambua duniani ni mapito tu ya watu.
Kwa upande wake Dk. Slaa na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi,
Jeams Mbatia walisema ipo haja kwa serikali kuyachukulia matukio hayo kwa uzito
kwani kinachoonekana ni upepo mpya wa kuhujumu dhidi ya viongozi wa dini.
Dk. Slaa, alisema
serikali haipaswi kuendelea kuiamini matukio hayo yanakuja kwa nguvu za Mungu
pekee bali ni mambo ambayo yanahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina kwani
haiwezekani kukawa na muendelezo wa hujuma kwa viongozi wa dini.
Hata hivyo,aliwataka waumini wa dini ya kikrosto na
wananchi wa Zanzibar , kuendeleza kuishi kwa amani ili kuifanya Tanzania kubaki
kuwa yenye amani.
Mbatia kwa upande wake alisema matukio ya kuhujumiwa
viongozi wa dini ni mambo ambayo serikali inapaswa kuyaangalia upya kama
inafanya uzuri katika kuimarisha utawala bora na kulilaumu jeshi la polisi
kutoweka ulinzi wa haraka nyumba za ibada.
Alisema katika kulishughulikia suala hilo tayari hivi
sasa vyama vya siasa kupitia Baraza linaloshugulikia vyama vya upinzani katika
kusimamia amani nchini vinakusudia kukaa pamoja na wadau mbali mbali ili kutafuta
njia ya amani kuinusuru Tanzania kuingia katika mizozo isiyokuwa na maana.
Maziko hayo pia yalihudhuriwa na Mabalozi mbali mbali
waanaoziwakilisha nchi zao Tanzania, akiwemo Balozi wa Ubelgiji, Balozi Mdogo
wa Norway mwenye makaazi yake Zanzibar na Maaskofu kutoka mikoa mbali mbali ya
Tanzania ukiwemo wa Kigoma, Tanga, Dodoama, Geita na Askofu Mkuu wa Jimbo la
Dar es Salaam.
Mapema akisoma wasifu wa marehemu Mushi, Askofu Cosmas Shao, alisema Padri Mushi alizaliwa Juni 15, 1957, kijiji cha Uru Kimanganuni, Mkoani Kilimanjaro ambapo baba yake ni Gabriel Wariro Andrea na mama yake ni Febronia Selemani Joseph.
Baada ya kuhitimu masomo ya elimu ya juu ya sekondari
mwaka 1976, alijiunga na seminari kuu Kibosho alikopata elimu ya falsafa, 1978
na 1979 na mwaka 1980 alingia seminari kuu ya Mtakatifu Paulo, Kipalapala –
Tabora, alikopata elimu ya tauhidi hadi mwaka 1982.
Baadae alirudi jimboni kwake Zanzibar 1983, na mwaka uliofuata 1984 aliendelea na masomo
yake huko Kipalapala na mnamo Julai 15, 1984 alipata daraja la Ushemasi katika
Parokia ya Bikira Maria wa Rosari, Kitope na Disemba 2,1984 akapewa daraja la
Upadre na Mhashamu Baba Askofu Bernard Martin Ngaviliau, katika kanisa kuu la
Mt. Yosefu Minara Miwili Zanzibar.
Aidha, alisema maisha yake akiwa Padre Mei 01, 1985
aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Rosari, Kitope, 1988 –
Paroko, Parokia ya Moyo Safi wa Maria Wete Pemba, 1991 – Paroko, Parokia ya Mt.
Antoni wa Padua Machui, 1995 – alipelekwa AMECEA PASTORAL INSTITUTE GABA,
Eldoret Kenya, kwa masomo ya Kichungaji.
Mwaka 1997 – 2003 alipelekwa masomoni Marekani na
kutunukiwa shahada ya uzamili, 2004 alipelekwa Gombera kituo cha Hekima Cheju, 2006 – Paroko, parokia ya Bikira Maria
wa Rosari Kitope. Machi 01, 2008 –
Paroko Kanisa Kuu la Mt. Yosefu, Minara miwili.
Disemba 02, 2009 aliadhimisha Yubilei ya Fedha, miaka 25
ya upadre, na vile alifanya kazi nyingine akiwa ni Mkurugenzi wa Idara ya
Maendeleo jimbo, mlezi wa magereza na jeshi la wananchi, Mratibu wa Huduma za sfya Jimbo.
No comments:
Post a Comment