Habari za Punde

Munir ajitosa tena urais ZFA . Asema ameshajua ujanja wa kupata ushindi

Na Mwajuma Juma
MWANDISHI wa habari mwandamizi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten hapa Zanzibar Munir Zakaria, ametangaza nia ya kugombea nafasi ya urais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), iliyoachwa wazi baada ya kujiuzulu kwa Amani Ibrahim Makungu mapema mwaka huu.


ZFA inakusudia kuendesha uchaguzi mdogo kupata Rais mpya atakayemrithi Makungu katika tarehe itakayotajwa baadae.

Kama Zakaria atachukua fomu na kuwania kiti hicho, hiyo itakuwa mara ya pili kwa mwanahabari huyo kujitosa kwenye kinyang’nyiro hicho.

Mara ya kwanza ilikuwa mwezi Disemba 2010, wakati aliposhiriki uchaguzi mkuu wa ZFA uliofanyika uwanja wa Gombani Pemba, ambao Rais aliyejiuzulu kabla ya Makungu Ali Ferej Tamim, aliweza kutetea nafasi yake.

Katika uchaguzi huo wa mwaka 2010, Zakaria aliambulia kura mbili tu nyuma ya Ferej aliyeshinda kwa kura 32 na Suleiman Mahmoud Jabir aliyepata kura 20.

Akizungumza na waandishi wa habari, Zakaria alisema kuwa, bado hajachoka kuomba
nafasi hiyo na mwaka huu ana matumaini makubwa ya kuweza kushinda.


“Ninajitokeza kuomba nafasi hii kwa mara ya pili tena, na mara hii natarajia sana kushinda katika uchaguzi huo kwani nimeshazijua njia za kupita na kupata kura tafauti na mwaka 2010
niligombea nikiwa nje, lakini tayari nimepita ndani ya ZFA ingawa nilitolewa kwa mizengwe”, alisema.


 
Alisema kazi kubwa anayokwenda kuifanya ZFA wakati akiwa Rais, ni kuondosha virusi vyote vilivyomo ndani ya chama hicho na
kuisafisha, na kamwe hataruhusu nyadhifa ambazo hazimo katika katiba kutumika ndani ya chama hicho.


 
“Tunataka kuibadilisha ZFA, na mara hii ni vyema Rais atoke nje ya kamati tendaji au katika wale ambao hawapigi kura”, alisema.

Alieleza kuwa, iwapo atachaguliwa, atapanga mikakati imara itakayoiwezesha ZFA kuwa kitu kimoja na serikali, na hatakuwa
tayari kuruhusu migogoro baina ya chama na serikali.

Alitaja baadhi ya mikakati hiyo, ni kumtumia kikamilifu Katibu wa chama ambaye ameteuliwa na serikali, na kuondosha nafasi ya Kaimu Katibu Mkuu ambayo haimo katika katiba wala kanuni za chama hicho.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.