Na: Hassan Hamad, OMKR
Wazee wa zamani wanatueleza kuwa wao walikuwa wakitumia misumeno ya kukereza, mapanga na mashoka kwa ajili ya kukata miti ya kujengea, kuni na hata kwenye viwanda vya kuchongea samani za majumbani. Wanasema kazi hii ilikuwa ngumu kwani walikuwa wakitumia nguvu za ziada na muda mwingi kuweza kukata gogo au mti mmoja, lakini ilikuwa rafiki wa mazingira na hakukuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira kama ilivyo sasa.
Katika miaka ya hivi karibuni kumeibuka misumeno ya moto ambayo hutumika kukatia miti na magogo kwa urahisi na kwa kutumia muda mdogo sana. Kwa kukisia ekari moja ya misitu inaweza kukatwa kwa chini ya saa moja kwa kutumia misumeno ya moto isiyozidi mitatu.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar Affan Othman Maalim, hivi karibuni alimueleza Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad kuwa takriban ekari 1000 za miti hupotea kila mwaka visiwani Zanzibar kutokana na kukatwa ovyo na kuongezeka kwa kasi hiyo kutokana na matumizi ya misumeno ya moto.
Tukiitathmini kwa umakini hali hii, tunagundua kuwa pamoja na na kuwa misumeno hii inarahisisha kazi na ukataji wa miti na magogo kwa shughuli mbali mbali, lakini inaelezwa kuwa ni adui mkubwa wa mazingira yetu. Hapa tunaweza kuhoji ikiwa wastani wa ekari 1000 za misitu zinaangamia kila mwaka visiwani Zanzibar, baada ya miaka 20 ijayo hali ya mazingira yetu itakuwaje?
Kwa kuzingatia kuwa nchi yetu ni ya Visiwa na uharibifu wa misitu utokanao na misumeno ya moto unaendelea siku hadi siku, ndio maana Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akashiriki moja kwa moja katika kampeni ya kutokomeza misumeno hiyo Zanzibar, baada ya kuichoma moto misumeno 23 hadharani huko Kizimbani Wete Pemba.
Kabla ya hapo, tayari misumeno 13 ilishaangamizwa kwa kuchomwa moto katika awamu mbili tofauti. Katika operesheni hiyo ya kuiangamiza misumeno 23, misumeno 4 zaidi iliachwa na kuhifadhiwa na Wizara ya kilimo kwa matumizi maalum ya dharura kama vile shughuli za uokozi wakati wa majanga, usalama barabarani na shirika la umeme. Hata hivyo Affan alisema misumeno hiyo itakuwa chini ya uangalizi wa Wizara ya Kilimo na Maliasili, na kwamba itatolewa kwa kibali maalum na kwa kazi maalum.
“Misumeno hii ni adui sawa na bunduki, kwa hivyo hairuhisiwi kwa mtu yoyote kuwa nayo bila ya kupata kibali maalum kutoka kwa mamlaka zinazohusika”, alifahamisha Affan.
Kutokana na hali hiyo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad wakati akiichoma misumeno 23, aliwasisitiza wananchi kushirikiana kuisaka misumeno ya moto ipatayo 276 ambayo inakadiriwa kuwepo katika visiwa vya Unguja na Pemba. Kati ya misumeno hiyo 150 inakadiriwa kuweko katika kisiwa cha Pemba na 126 katika kisiwa cha Unguja.
Alisema iwapo wananchi watashirikiana hasa kupitia kwa masheha na vikundi vya polisi jamii, misumeno hiyo inaweza kukamatwa na kuangamizwa kabisa, na kubakia ile michache inayodhibitiwa na Wizara ya Kilimo kwa kazi maalum.
“Kila mtu ana wajibu wa kuwafichua watumiaji wa misumeno hii, lakini mashena na polisi jamii muna jukumu kubwa zaidi, na nina hakika mukiamua munaweza kuwabaini wote wenye misumeno ya moto”, alifahamisha Maalim Seif.
Katika majumuisho ya ziara yake ya siku mbili kwa Wizara ya Kilimo na Maliasili yaliyofanyika ukumbi wa kituo cha amali Vitongoji Chake Chake Pemba, Maalim Seif alisema si vibaya ikiwa Wizara hiyo itafikiria kutangaza tunzo maalum kwa watu watakaoamua kuisalimisha misumeno hiyo au watakaofanya juhudi za kupatikana kwake.
Naibu Waziri wa Kilimo na Maliasili Mtumwa Kheir Mbarak ambaye alijumuika na Makamu wa Kwanza wa Rais katika ziara na operesheni hiyo, alisema misumeno hiyo imekuwa adui wa muda mrefu kwa mazingira yetu, na inaweza kuifanya nchi kuwa jangwa kwa muda mfupi, na kwamba ni hatari hata kwa afya ya binadamu.
“Niliwahi kupewa kesi moja ya mtu aliyekatwa na msumeno wa moto, nilitokwa na machozi baada ya kumuona amekatwa miguu yake yote miwili kutokana na msumeno huo, inasikitisha sana”, alieleza Naibu Waziri huyo huku akitilia mkazo haja ya kuiangamiza misumeno hiyo.
Wakati umefika sasa tushirikiane kuisaka misumeno ya moto popote ilipo Zanzbar na kuiangamiza kabisa, sambamba na kudhibiti uingizwaji wa misumeno hii nchini. Inawezekana ikiwa kila mmoja atatekeleza wajibu wake ipasavyo.
No comments:
Post a Comment