Yataka ‘Sports Michezo’ ya ZBC isiwachambue bila kuwepo
Na Salum Vuai, Maelezo
WADAU wa soka wa Zanzibar, wameibua mjadala juu ya hatua ya Chama cha Soka Zanzibar kuitaka televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar, isiwaite kuchambua masuala ya chama hicho kupitia kipindi cha ‘Sports Michezo’ bila wenyewe (ZFA) kuwepo.
Kipindi hicho maalumu huandaliwa na mwanahabari Farouk Karim na kurushwa kila siku ya Jumamosi mnamo saa 3:00 usiku.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tafauti, wadau hao wamedai kuwa, ZFA si chama cha watu wa kundi fulani bali ni cha wananchi wote na kwamba wana haki kukijadili bila masharti yoyote.
Kocha wa mabingwa wa soka Zanzibar KMKM Ali Bushiri Mahmoud, ameeleza kuwa, kama watu watakutana kuzungumzia masuala ya mpira wa miguu nchini, ni lazima pia watakigusa chama hicho kwa kuwa ndicho kilichopewa dhamana.
Alisema, hatua hiyo inaonesha woga wa chama hicho, na viongozi wake kutokuwa tayari kukosolewa wala kushauriwa, pale wanapofanya mambo kinyume na matarajio ya wananchi na wadau wa soka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wazee Sports Salum Bausi Nassor, amesema ingawa hafu4rahishwi na uamuzi huo, yuko tayari kukaa pamoja na viongozi wa chama hicho wakati wa kipindi cha ‘Sports Michezo’ ili kila upande uoneshe changamoto zinazolikabili soka la Zanzibar.
“Mimi ninafahamu kuwa mara nyingi viongozi wa ZFA huitwa katika kipindi hicho, lakini wanakwepa wakitoa sababu mbalimbali, sasa kwani nini sisi tusizungumzmie soka letu mpaka wao wawepo? alihoji Bausi.
Naye Hussein Ali Ahmada, mmoja wa waasisi wa Akademi ya kuibua na kukuza vipaji ya Oranje iliyoko Kikwajuni, alisema haoni sababu ya msingi kulazimisha kuwepo kwa viongozi wa ZFA katika kipindi hicho, kwani wanaweza kujadiliwa na baadae wakipoenda waombe muda wa kujibu kama wanayo majibu.
“Tatizo ninaloliona, ni kwamba viongozi hao wanataka wapambwe kwa sifa nzuri hata ale wanapofanya madudu yanayochangia kuporomosha soka la Zanzibar. Hawataki maovu ao yaanikwe na wala hawataki kubadilika”, alieleza.
Muandaaji wa kipindi hicho Farouk Karim, alisema analazimika kuheshimu uamuzi wa ZBC, lakini akadai mara nyingi amekuwa akiwaita viongozi wa ZFA lakini wanapiga danadana.
Aidha, alisema kimsingi, ZBC na ZFA zote ni mali za wananchi ambao wameonesha kuvutiwa na kipindi hicho, ambacho huwa kinajadili mada nzito na muhimu inayokuwepo kwa wakati maalumu kuhusiana na maendeleo ya michezo.
Baada ya baadhi ya wadau kudai kuwa Kaimu Rais wa ZFA Haji Ameir Haji ameitaka ZBC iwazuie wafanyakazi wake kuichambua ZFA kupitia ‘Sports Michezo’, Ameir amedai alichoomba ni kutaka wasijadiliwe bila wenyewe kushiriki mjadala wowote unaowahusu.
Aidha aliwashutumu wadau hao kuwa wanatumiwa kuibomoa ZFA, na kuongeza kwamba Jumamosi wiki hii yuko tayari kuitwa pamoja nao katika kipindi hicho ili kuzungumzia mambo yahusuyo soka hapa nchini.
Alipoulizwa Mkurugenzi wa ZBC Hassan Abdallah Mitawi, alikiri kuwa Haji Ameir alikwenda ofisini kwake kupeleka madai ya kubomolewa ZFA na wadau, lakini hawakuzuiwa kuijadili, bali ameagiza wakati wa kipindi hicho, nao waitwe ili kupewa haki ya kujibu kama walivyoomba.
No comments:
Post a Comment