Na Mwandishi wetu, Dodoma
KWA mara nyengine tena vurugu zimeshuhudiwa Bungeni wakati msemaji wa kambi ya upinzani wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ezekiah Dibogo Wenje, akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Vurugu hizo zilimlazimu Naibu Spika Job Ndugai kusitisha kikao cha Bunge hadi jana jioni.
Ghasia ziliibuka baada ya Wenje kusema Chama cha Wananchi CUF kinapigania haki ya ndoa za jinsia moja, ushoga na usagaji.
Hali hiyo ilisababisha Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdalla Salim (CUF) kusimama na kuomba mwongozo Spika, akitaka maneno yaliyomo kwenye ukurasa wa nane wa hotuba ya kambi ya upinzani yaondolewe kwa sababu yanaudhi na yanakashifu chama hicho.
Akizungumzia kipengele cha vyama vya siasa na misaada kutoka nje ya nchi, Wenje alisema pamoja na misaada ambayo vyama vya siasa vinapata kutoka serikali hii ya CCM bado vyama vya siasa vimekuwa na mahusiano na baadhi ya vyama vingine vya siasa katika mataifa ya magharibi.
Alisema vyama hivyo vimekuwa vikipokea misaada ya aina mbalimbali kama fedha, nyenzo na mengineyo kadiri ya makubaliano na mirengo ya kiitikadi ya vyama husika.
Alisema pamoja na ukweli huo bado vipo vyama vya siasa vinavyopotosha umma kuhusiana na misaada vinayopokea kutoka nje ya nchi na vyama hivyo vimekuwa mstari wa mbele kueneza propaganda za uongo kuwa vyenyewe havipokei misaada kutoka nchi za magharibi.
Alisema CCM ‘wanajiita’ kuwa wapo mrengo wa kijamaa na kikomunisti na wamekuwa wakipokea misaada mingi ya fedha na nyenzo kutoka umoja wa vyama vya kikomunisti ulimwenguni kutoka nchi kama Ujerumani kupitia SDP ,Uingereza kupitia chama cha Labour,China kupitia chama cha Kikomunist na Marekani kupitia chama cha Democrats.
Alisema pamoja na misaada ya kifedha na kiufundi ambayo CCM imekuwa ikipata kutoka nje wamekuwa hawatangazi hadharani hata mara moja kuhusiana na kiasi ambacho wamekuwa wakipokea na hivyo kila kitu kwao imekuwa ni siri kuu ya viongozi wao.
Alisema kwa upande wa chama cha CUF, kutokana na itikadi zake za mrengo wa Kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni pamoja na “kupigania haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji na ushoga,” CUF kimekuwa kikipata msaada wa kifedha na nyenzo nyingine mbalimbali kutoka kwa vyama vya mrengo wa kiliberali na msaada wa mwisho ni hivi majuzi mwezi Machi 2013 waliposaini makubaliano na chama cha Kiliberali kutoka Norway.
Lakini kwa upande wa chama chake cha Chadema, wapo kwenye umoja wa vyama vya kidemokrasia , ambavyo msingi wake ni pamoja na kuwa na familia, kama taasisi muhimu katika jamii, na kusema: “tunapinga vitendo vyote vya ushoga na usagaji.”
Baada ya kauli hiyo, Wabunge wengi wao kutoka CUF walisimama wakimtaka Naibu Spika amzuie Wenje kusoma bajeti yake.
“Ondoa uchafu wako, kama hamna heshima nyinyi tu sisi tuna heshima zetu,” walisema Wabunge hao kwa hasira.
Na pale Ndugai alipolazimisha kumruhusu Wenje kuendelea kusoma bajeti, Wabunge waliendelea kugonga meza na kupaza sauti wakisema hotuba hiyo haisomeki hadi maneno hayo yaondolewe.
Wabunge walionesha hasira kali na wengine wakijaribu kumvamia Wenje huku baadhi yao wakionekana kuwazuia.
Baada ya kuona vurugu zinazidi, Naibu Spika alilazimika kusitisha shughuli za bunge kabla ya muda wake wa kawaida, hadi jana jioni na kutaka kamati ya maadili ikutane.
Ilipofika jioni Kamati ya Maadili chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Kapteni John Chiligati alisema kamati ilimsikiliza mlalamikaji (Salim) na mlalamikiwa (Wenje) kwa lengo la kuwasikiliza ili kuchukua hatua.
Alisema Kamati ilijiridhisha maneno hayo yalikuwa ya kuudhi, ya kudhalilisha na ambayo hayafai hata kuandikwa.
Hivyo, Kamati ilimtaka Wenje aondoe maneno hayo na kwa sababu maneno yaliudhi na kuchefua upande mwengine aombe radhi.
“Tulishauri yale maneno yafutwe, yaondolewe kwa sababu hiyo nia nje aliyosema imeleta kichefuchefu ameumiza watu wengine, kuna watu wamepata maumivu basi aombe radhi,” alisema Chiligati.
Wenje alikubali ombi la Kamati la kuondoa maneno hayo lakini alikataa kuomba radhi na hata pale alipoleta mabadiliko mbele ya Kamati, maneno hayo hakuyaondoa.
Hali hiyo ilimlazimu Naibu Spika kumlazimisha Wenje atekeleze ombi la kamati, lakini alionesha kiburi na kukataa amri ya Spika.
Na Massoud alipotakiwa kuzungumza, alisisitiza kwamba kama maneno hayo hayatondolewa, hotuba ya upinzani haitasomwa.
Baada ya kuona mazingira ya kuongoza kikao ni magumu, Naibu Spika alisitisha tena shughuli za bunge hadi kesho na suala hilo kulirejesha tena kwa Kamati ya Maadili ili kuangalia hatua za kuchukua.
No comments:
Post a Comment