Na Abdi Suleiman, Pemba
BAADA ya juzi kuwakimbia mashabiki wanaofika kuangalia mazoezi yao, timu ya Yanga jana imerejea katika uwanja wa Gombani kuendelea na mazoezi kikamilifu uwanjani hapo. Juzi, wachezaji wa timu hiyo, waliwaacha solemba mashabiki na kwenda kufanya matembezi maeneo ya Vitongoji, kuangalia mandhari ya kijani katika kisiwa hiki cha harufu ya marashi ya karafuu, na kuwafanya wapenzi wao kuhaha wasijue wapi walipokuwepo.
Mashabiki wengi walijitokeza jana asubuhi kuangalia namna wanandinga hao wanaonolewa na Mholanzi Ernie Brandts wanavyojifua kujiandaa kuua mnyama Simba SC, Mei 18, mwaka huu.
Baadhi ya wapenzi wa Yanga waliozungumza na gazeti hili, walisema ubingwa bila kumuua mnyama hautakuwa na ladha, hivyo ni lazima Simba ikubali kipigo ili kunogesha mafanikio yao ya msimu huu.
Mmoja wa wadau wa soka kisiwani hapa, Mohammed Salum Ali, mkaazi wa Kisiwani kwa binti Abeid, alisema ujio wa timu hiyo umewapa faraja kwani muda mwingi walikuwa wakiiona katika televisheni tu. Mchezaji wa Yanga, Mrwanda Haruna Niyonzima, alisema kambi yao hiyo inatia matumaini makubwa kwamba Simba haina pa kutokea, na lazima ikubali kufa.
Aliwataka mashabiki wao kukaa tayari kusheherekea ubingwa wao wa ligi kuu msimu wa mwaka 2012/2013, baada ya kuwafunga mahasimu wao wa jadi Simba hiyo Mei 18 uwanja wa Taifa. Naye Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Fred Felix ‘Minziro’, alisema amesikitishwa sana na taarifa za baadhi ya vyombo vya habari jana, kwamba kiungo wao Haruna Niyonzima ameondoka, akidai kuwa si za kweli. Wakati Yanga iko Pemba, watani wao Simba, wamejichimbia kisiwani Ungjuja na tayari wameanza mazoezi kwa lengo la kutibua sherehe za ubingwa Jangwani.
No comments:
Post a Comment