Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI ya vinywaji vya Coca-Cola, imelikabidhi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mipira na vizibao (bips), kwa ajili ya timu zinazoshiriki mashindano ya soka ya vijana ya Copa Coca-Cola mwaka huu.
Kuanzia mwaka huu, mashindano hayo yatashirikisha wachezaji wenye chini ya miaka 15 badala ya 17 kama ilivyokuwa miaka iliyopita.
Lengo la kubadili umri kama ilivyoshauriwa na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), ni kuweza kuwafikia vijana wadogo zaidi na hivyo kuwa na wigo mpana wa kukuza vipaji vyao kwa muda mrefu zaidi kabla hawajachukuliwa na klabu kubwa.
Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo ilifanyika ofisi za Coca-Cola Tanzania jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Vifaa vilivyotolewa na Coca-Cola na kupokelewa na Ofisa Maendeleo ya soka wa TFF, Salum Madadi, vitatumika ngazi ya wilaya. Akipokea vifaa hivyo, kocha huyo wa zamani wa Simba SC na Taifa Stars, amewataka viongozi wa soka ngazi ya wilaya na mikoa kuzingatia kanuni na taratibu za Copa Coca-Cola. Alisema kuwa baadhi ya wilaya tayari zimeshaanza mechi za michuano hiyo ya vijana na kuzitaka wilaya zilizokuwa zikisubiri vifaa ili kuanza kucheza, kufanya hivyo mara moja kwa kuwa sasa vifaa viko tayari.
Meneja Bidhaa wa Coca-Cola Tanzania Maurice Njowoka, alisistiza msimamo thabithi wa Coca-Cola wa kuendelea kudhamini mashindano hayo ambayo yamekuwa chimbuko la wanasoka chipukizi nchini Tanzania.
Barani Afrika, mashindano ya soka ya vijana ya Copa Coca-Cola hufanyika katika nchi zaidi ya 20 na kushirikisha zaidi ya wachezaji chipukizi zaidi ya 50,000.
No comments:
Post a Comment