Haji Nassor na Abdi Suleiman, Pemba
MGOMBEA wa CUF, Yussuf Salim amechaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Chambani kisiwani Pemba katika uchaguzi mdogo uliofanyika jana.
Salim anarithi nafasi iliyoachwa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Hemed Salim Khamis (CUF) aliyefariki dunia mwezi Machi mwaka huu.
Mbunge huyo mteule alipata kura 2708 sawa na asilimia 83.68 na kuwashinda wapinzani wake Mattar Zahran (CCM) aliyepata kura 402 sawa na asilimia 12.42, Said Miraj wa ADC aliyepata kura 114 sawa na asilimia 3.52 na mgombea pekee mwanamke kutoka CHADEMA, Siti Ussi Shaib aliepata kura 12 sawa na asilimia 0.37.
Akitangaza matokeo hayo katika kituo cha mafunzo ya ualimu Mizingani, Msimami wa Uchaguzi Mohammed Rashid Abdalla alisema walioandikishwa kupiga kura walikuwa watu 4,834 na waliopiga kura walikuwa watu 3,255.
Alisema kura halali zilikuwa 3,236 na kurffa 19 ziliharibika.
Msimamizi huyo alimtangaza mgombea wa CUF kuwa mshindi katika uchaguzi huo, uliofanyika katika mazingira ya amani ya kutosha.
Wakizungumza muda mfupi kabla ya matokeo kutangazwa, wagombea wote walisifia jinsi uchaguzi huo uliovyoendeshwa na kwamba kama uchaguzi mkuu utaendeshwa katika mazingira hayo, Zanzibar inaweza kuwa kama Ulaya.
Aidha waliahidi kukubali matokeo yoyote yatakayotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC).
Uchaguzi huo uliendeshwa kwa utulivu mkubwa ambapo baada ya wananchi kupiga kura walielekea nyumbani kwenda kuendelea na shughuli zao za kawaida na hata wale polisi waliokuwepo katika vituo vya kupigia kura walijikuta wakiwa hawana kazi.
Msaidizi Msimamizi wa Uchaguzi NEC, Jimbo hilo Hussein Zubeir Maziku, alisema uchaguzi kwa ujumla ulifanyika katika mazingira ya amani na hakuna dosari zozote za kiutendeji ziliziojitokeza.
Mmoja ya wapiga kura,Abdi Juma Mohammed (55,) aliyepiga kura kituo cha Ngwachani, alisema uchaguzi ulikuwa mzuri na utulivu ulitawala wakati wote.
Mwanaisha Kombo Khamis (45) ambae nae alipiga kura kituo cha Ngwachani, alisema uchaguzi uliitishwa katika mazingira ya shwari na watu wasiojiweza walipata usaidizi wa kutosha.
Nae Asha Abdalla Hassani (30) mpiga kura wa kituo cha Mizingani , alikiri kutokuwepo matatizo yoyote kwa sababu watu wa Chambani wote ni wamoja.
Khadija Khamis Khatib (60) mpiga kura kituo cha Ukutini, alisema walipiga kura bila usumbufu wowote na kila mmoja alirudi nyumbani baada ya kutekeleza haki yake ya kikatiba.
Mgombea wa CUF, Yussuf Salim Hussein, akizungumza baada ya kupiga kura alisifu jinsi uchaguzi huo ulivyoondeshwa kwani kila mmoja alipata kutekeleza haiki yake.
Aidha Naibu Mrajisi wa Vyama vya Siasa Tanzania, Rajab Baraka Juma, alisema hali ya uchaguzi katika jimbo la Chambani, ulikwenda vyema na kwamba ulinzi uliimarishwa ingawa hakukuwa ghasia zozote.
Hadi kufikia majira ya 7:00 mchana baadhi ya vituo vilikuwa vitupu na vyengine kuliwa na mpiga kura mmoja mmoja.
No comments:
Post a Comment