Habari za Punde

Mawakili kesi ya mauaji ya watu 229 wataka iondolewe. Ni ya kuzama Mv. Spice Islanders

Na Khamis Amani
MAWAKILI wanaowatetea washtakiwa 12 wa mauaji ya watu 229 bila kukusudia, wameiomba mahakama kuu kuiondoa kesi hiyo, kwa kuwa upande wa mashtaka haujawa tayari.

Mawakili hao wakiongozwa na Abdalla Juma, walidai upande wa mashtaka unatakiwa kujipanga tena upya na baadae kurejea tena mahakamani kuendelea na kesi.

Madai hayo ya mawakili hao yalikuja baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati mpya ya mashtaka, ambayo imeongeza idadi ya watu waliofariki kutoka 228 hadi 229, kufuatia kuzama kwa meli ya MV.Spice Islanders katika mkondo wa Nungwi ilipokuwa ikenda Pemba ikitokea Unguja.

Mawakili hao, walidai wanavyojua utaratibu wa kurekebisha hati ya mashitaka hufanywa kwa taratibu za kisheria.

"Mheshimiwa marekebisho hufanywa kwa matakwa ya mahakama chini ya kifungu cha 250 (2), kifungu hicho kipo wazi kabla ya kusikiliza mahakama itatoa maelezo na kutoa amri ya kufanya mabadiliko ikiona ipo haja hiyo," ulidai upande wa utetezi, mbele ya Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, anaesikiliza kesi hiyo.

Hiyo ni takriban mara ya pili kwa washitakiwa wa kesi hiyo kubadilishiwa hati ya mashitaka tokea kufikishwa mahakamani hapo.

Ubadilishwaji wa hati hiyo ni kutokana na madai ya upande wa mashitaka kwamba hati iliyopo hivi sasa ina mapungufu ya kisheria.

Ombi la kubadilishwa hati hiyo ya mashitaka liliwasilishwa na jopo la mawakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ali Khaidar na Slim Said wakioongozwa na Omar Sururu Khalfani.

Waliiomba mahakama hiyo kukubali kupokea hati mpya ya mashitaka ya kesi hiyo, kutokana na mapungufu ya kisheria yaliyopo katika hati iliyopo sasa.

Mabadiliko hayo yamefanywa kwa mujibu wa kifungu cha 250 (1) cha sheria za mwenendo wa jinai namba 7/2004 sheria za Zanzibar.

Baada ya vuta nikuvute hiyo,Jaji Makungu alikubaliana na hoja za upande wa mashitaka na kukubali kuipokea hati hiyo mpya ya mashitaka, kutokana na kwamba hoja ya mapungufu hayo tayari yameshatolewa na Wakili Hamid Mbwezeleni wa upande wa utetezi katika kikao kilichopita.

Baada ya maamuzi hayo ya mahakama, upande wa mashitaka uliikabidhi mahakama pamoja na upande wa utetezi hati mpya ya mashitaka na kuwasomea washitakiwa mashitaka yao yanayowakabili ambayo hata hivyo kwa mara nyengine tena wameyakana.

Katika hati hiyo mpya, washitakiwa hao wameshitakiwa kwa kuua bila ya kukusudia chini ya vifungu vya 195 na 198 vya sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar, badala ya kifungu cha 195 pekee walichoshitakiwa katika hati ya zamani.

Aidha hati hiyo, imewataja washitakiwa kwa umri, makaazi pamoja na vyeo na dhamana walizonazo ikiwa ni tofauti na hati iliyopita iliyowataja kwa majina pekee.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 23 mwaka huu kwa kutajwa na washitakiwa wote hao wapo nje kwa dhamana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.