Na Mwandishi wetu, DSM
ULINZI umeimarishwa maradufu katika jiji la Dar es Salaam, wakati huu ambapo Rais wa taifa kubwa duniani, Barack Obama wa Marekani akitarajiwa kutembelea Tanzania kwa mara ya kwanza tokea awe Rais.
Rais Obama na familia yake yuko nchini Senegal katika kituo chake cha kwanza cha ziara yake ya siku tano barani Afrika.
Magari ya polisi yamekuwa yakirandaranda katika maeneo mengi ya jiji hilo huku askari kanzu wakionekana kwa wingi katika maeneo ambayo kiongozi huyo atapita na katika hoteli kubwa.
Aidha wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu machinga wamedhibitiwa na hali usafi katika jiji hilo imeimarishwa.
Kamanda wa polisi mkoa maalum wa Dar es Salaam, Suleiman Kova ameonya kuwa polisi itawadhibiti na kuwachukulia hatua kali wale watakaojaribu kuvuruga amani wakati wa ziara hiyo.
Aidha alisema maandamano ya CUF yaliyopangwa kufanyika kesho yamepigwa marufuku ili kutoa nafasi kwa polisi kushughulikia ujio wa kiongozi huyo.
Alisema mbali na ujio wa Obama, Tanzania ni mwenyeji wa mkutano wa ushirikiano kwa manufaa ya wote (Smart Partnership Dialogue) unaowakutanisha viongozi wa mataifa mbali mbali na washiriki wapatano 800, hivyo polisi hawatatoa mwanya wa kuvurugwa amani.
Aidha alisema polisi ina taarifa za kiintelejesia kwamba kuna makundi ya wanaharakati na viongozi wa kisiasa walioandaa mabango wakati wa ziara ya Obama, lakini akaonya kwamba polisi itawashughulikia watu hao.
Ujio wa Obama umevuta hisia za wengi huku tayari mahoteli mengi yaliyopo jijini Dar es Salaam yakiwa yameshafurika wageni.
Aidha makachero wa Marekani pamoja na vifaa vya ulinzi ikiwemo meli inayobeba ndege imeshawasili katika bahari ya Hindi kusaidia kufanikisha ziara ya kiongozi huyo.
Aidha magari 14 yatakayotumiwa na kiongozi huyo, yanatarajiwa kuwasili wakati wowote chini ya ulinzi mkali wa makachero wa Marekani.
Ziara ya Obama katika ukanda wa Afrika Mashariki inatarajiwa kuinufaisha Tanzania kiuchumi na kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.
No comments:
Post a Comment