Habari za Punde

Wafanyakazi ZSTC wahusishwa na magendo ya karafuu

Na Masanja Mabula, Pemba
WAKULIMA wa zao la karafuu katika Mkoa wa Kaskazini Pemba wametaka watendaji wa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) kuchunguzwa kwani baadhi yao ndio wanaochangia kuwepo na magendo ya karafuu.

Wakizungumza katika mktano uliofanyika ukumbi wa Jamhuri Wilaya ya Wete kisiwani Pemba, walisema baadhi ya watendaji wa shirika hilo wamekuwa wakitoa pesa na kuwapa wanunuzi wa karafuu na kupita kwa wakulima kununua karafuu.

Akichangia katika kikao hicho, Khamis Abdalla Chande (78) mkaazi wa Mtambwe, alisema kumezuka mtindo wa watu kununua karafuu mbichi kwa kikombe huku pesa za kuendeshea biashara hizo zikitolewa na watendaji wa ZSTC ambao sio waaminifu.

"Tunaiomba serikali iwachunguze watendaji wake, kwani wapo baadhi yao wanatoa fedha na kuwapa wanunuzi na kupita wakinunua karafuu vijijini, hali hii itaendelea kuinyima mapato serikali ," alisema.

Naye Suleiman Juma Khalfan (45) wa Mgogoni Wilaya ya Micheweni alisema bado serikali haijaweka utaratibu mzuri wa kuilinda karafuu na mikarafuu, hali inayosababisha mikarafuu kuendelea kukatwa.

Alisema serikali inahitaji kuimarisha mikarafuu pamoja na ubora wa karafuu, lakini hilo halitawezekana iwapo hakutakuwa na sheria zitakazowabana na kuwapa adhabu kali wanaoharibu mikarafuu kwa makusudi.

Aidha Nwinyi Juma Hamad mkulima kutoka Gando alisema ni vyema vyombo vya ulinzi navyo vikafanyiwa uchunguzi na kupewa elimu ili kuacha kuwakumbatia wanaosafirisha karafuu kimagendo.

Pia ameishauri serikali kutunga sheria kwa ajili ya kuulinda mkarafuu mchanga unaopandwa ili usiharibiwe na wafugaji.

Mwenyekiti wa kikao hicho Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui alisema lengo na azma ya serikali ni kuboresha ubora wa karafuu na kuongeza wingi wa mikarafuu nchini.

Alisema hilo litawezekana iwapo wananchi watashirikiana na serikali kuhakikisha karafuu zinazozalishwa ni safi.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Juma Kassim Tindwa amewataka wakulima kuitumia fursa ya kuwepo mikutano inayoandaliwa na ZSTC kuibua na kueleza changamoto zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.