Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akimkabidhi Wino pamoja na mashine ya Fotokopi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi ya Vokokotoni Taifa Khamis Ahmed.
Mama Asha alikabidhi mchango huo kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya Skuli hiyo kuwazawadia wanafunzi waliofanikiwa kuingia mchepuo miaka mitatu iliyopita.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ
Na Othman Khamis Ame OMPR
Wakati mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ukimaliza kumi la mwanzo la Rehma na kuingia kumi la Pili la Maghafira waumini mbali mbali wa Dini ya Kiislamu wanaendelea na harakati zao za kufutari pamoja wakiwa katika makundi na daraja tofauti.
Utaratibu huo umo ndani ya Dini ya Kiislamu ukilenga kujenga ukaribu zaidi miongoni mwa waumini hao hali ambao huleta utulivu, upendo, uvumilivu na kuimarisha mapenzi baina yao.
Wazee wanaoishi katika nyumba zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya hifadhi yao zilizopo Mtaa wa Welezo na Sebleni wamepata faraja hiyo wakati walipokula futari ya pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi pamoja na baadhi ya Viongozi wa Serikali,Kisiasa na hata wale wa Dini.
Balozi Seif aliandaa futari hiyo kwa lengo la kuwa karibu zaidi na wazee hao ambao walitoa mchango mkubwa kwa taifa wakati wa harakati za kupigania ukombozi wa Visiwa hivi vya Unguja na Pemba.
Mkurugenzi Mohammed alisema hatua hiyo kwa kiasi kikubwa huleta faraja kwa wananchi hasa wazee wa Welezo na Sebleni ambao wako mbali na familia zao jambo ambalo huwaondoshea upweke.
Alishauri kwa baadhi ya Viongozi na watu waliojaaliwa uwezo kuunga mkono harakati hizo za kuwaandalia futari watu wasiojiweza na wale wenye kipato cha chini ili kupunguza daraja lililopo kati ya wenye uwezo na wale wasiokuwa na uwezo.
Ibada ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni miongoni mwa nguzo tano za Kiislamu zinazomuajibikia muumini wa Dini hiyo kuzitekeleza ambapo ile ya Hijja hupaswa kutekelezwa kwa yule muumini wenye kipato.
Wakati huo huo Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alikabidhi mchango wa mashine ya Fotokopi kwa ajili ya Skuli ya Msingi ya Vikokotoni pamoja na Shilingi Milioni 1,000,000/- kusaidia Madrasa ya Jeilan Islamia ya Mtaa huo.
Mchango huo ameukabidhi kwa uongozi wa Skuli na Madrasa hiyo hapo nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ukishuhudiwa pia na Uongozi wa Kamati ya Maendeleo ya Jimbo la Kikwajuni iliyoongozwa na Mwakilishi wake Mahmoud Mohammed Mussa.
Akikabidhi mchango huo Mama Asha Suleiman Iddi aliuomba Uongozi wa Skuli ya Vikokotoni kuwa waangalifu wakati wa matumizi ya mashine hiyo ili iweze kuwahudumia kwa kipindi kirefu zaidi.
Mama Asha alieleza kwamba licha ya majukumu mbali mbali yanayomkabili lakini aliuhakikishia uongozi wa Jimbo hilo kwamba yuko tayari wakati wowote kusaidia au kuchangia Maendeleo ya Wananchi popote pale hapa Nchini.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni Mahmoud Mohammed Mussa alisema Wananchi wa Jimbo hilo wanathamini juhudi anazoendelea kuchukuwa Mama Asha hasa katika utekelezaji wa ahadi anazozitoa.
Alifahamisha kwamba jambo hilo ni zito hasa ikizingatiwa kutekelezwa katika kipindi hichi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani ambacho kimejaa baraka na neema kwa wacha mungu.
Kwa upande wake Afisa Elimu na Mafunzo ya Amali Mkoa Mjini Magharibi Khatib Tabia Muhsin aliueleza mchango huo wa Mama Asha wa Mashine ya Fotokofi wenye thamani ya jumla ya Dola za Kimarekani Mia Tisa utasaidia nguvu za Wizara ya Elimu katika kuimarisha sekta hiyo Nchini.
Alisema Mashine hiyo kwa kiasi kikubwa itapunguza gharama za uchapishaji wa kazi za Walimu, wanafunzi na hata machapisho ya Mitihani ya majaribio kwa wanafunzi wa Skuli hiyo.
Ahadi ya Mama Asha Suleiman Iddi aliitoa kwa uongozi wa Skuli ya Vikokotoni na Madrasa ya Jeilan Islamia kwa karibu miaka mitatu iliyopita wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya skuli hiyo ya kuwapongeza na kuwazawadia wanafunzi wa skuli hiyo waliofanikiwa kuingia michepuo skuli mbali mbali.
No comments:
Post a Comment