Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya CRDB Dk.Charles Kimei,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na ujumbe wake leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Ujumbe wa Benki ya CRDB,ukiongozwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Dk.Charles Kimei,(wa pili kulia) alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
Na Said Ameir, Ikulu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuimarika kwa uzalishaji wa zao la karafuu kisiwani Pemba kunaongeza mahitaji ya huduma za kibenki katika kisiwa hicho.
Dk. Shein amesema hayo leo Ofisini kwake Ikulu wakati alipokuwa akizungumza na ujumbe wa Benki ya CRDB uliokuwa chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake Dk. Charles Kimei.
“Biashara ya karafuu sasa imerudi tena kisiwani Pemba na kukifanya kisiwa hicho kuchukua nafasi yake ya asili ya kuwa mzalishaji mkubwa wa karafuu Zanzibar” alisema.
Aliueleza ujumbe huo kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha zao la karafuu nchini ikiwemo utoaji huduma za ugani kwa wakulima wa zao hilo,kuwapatia wakulima miche ya mikarafu pamoja na kuwapatia bei nzuri ya karafuu kila inapowezekana.
Kwa hiyo Dk. Shein aliitaka benki hiyo kukipa nafasi muhimu kisiwa cha Pemba katika kusambaza huduma zake za kibenki humu nchini na kuupongeza uongozi wa benki hiyo kwa azma yake ya kuanzisha ofisi zake za kudumu Unguja na Pemba.
“Nimevutiwa na nia yenu ya kutaka kujenga Ofisi zenu Unguja na Pemba na hii ni ishara kuwa wananchi wameipokea vyema benki yenu na wamefurahia huduma mnazozitoa” alisema Dk. Shein na kueleza matumaini yake kuwa kuanzishwa kwa huduma za benki hiyo Zanzibar kutaongeza fursa zaidi kwa wakulima kupata huduma za benki ikiwemo mikopo.
Rais wa Zanzibar ametumia fursa hiyo kuipongeza Benki hiyo kwa mafanikio yake iliyoyapata hadi sasa ambapo kwa mujibu wa maelezo ya Mkurugenzi Mkuu wake ndani ya miaka mitatu benki hiyo imeweza kuweka dhamana ya shilingi 12 bilioni huku ikiwa imeshatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 11.
Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Dk. Charles Kimei amesema benki yake imedhamiria kuimarisha huduma zake katika visiwa vya Unguja na Pemba ili wananchi wengi zaidi waweze kufikia na kufaidika na huduma zake.
Dk. Kimei amemueleza Rais wa Zanzibar kuwa benki yake hivi sasa ina tawi moja tu mjini Unguja ambalo linafanya vizuri na kwamba mipango iko mbioni kuanzisha tawi jingine kisiwani Pemba pamoja na vituo vya wakala wa kutoa huduma za kibenki kote nchini.
“Biashara yetu hapa ni nzuri tuna wateja wazuri na ‘risk’ ya mikopo si kubwa hivyo tumeweza kutoa mikopo mingi na kuwafikia wateja wengi wakiwemo vikundi vya kuweka na kukopa-SACCOS pamoja na wakulima wa mwani”alisema.
Alifafanua kuwa benki hiyo kupitia ya kampuni yake ya kutoa mikopo midogomidogo na kushirikiana na SACCOS 9 zenye wanachama wapatao 5,000 na imeweza kutoa mikopo kwa wakulima wa mwani yenye thamani ipatayo shilingi bilioni 3.
Dk. Kimei alimhakikishia Rais wa Zanzibar kuwa benki yake itaendelea kuiunga mkono serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mipango yake mbali mbali ya maendeleo ikiwemo kusaidia uwezeshaji wananchi
No comments:
Post a Comment