WIZARA ya Afya Zanzibar, imeelezea kuridhishwa na misaada mbalimbali ya kiafya inayotolewa na Marekani na taasisi nyengine binafsi za nchi hiyo.
Naibu Waziri
wa Afya Dk. Sira Ubwa Mamboya, ameueleza ujumbe wa wasaidizi wa Maseneta kutoka
Marekani uliomtembelea ofisini kwake jana, kuwa mchango wa nchi hiyo umesaidia
sana kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa Unguja na Pemba.
Ujumbe huo
umewasili jana kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na
Marekani na mashirikia mingine ya misaada ya nchi hiyo katika sekta ya
afya.
Dk. Sira
alisema, misaada inayotolewa na nchi hiyo kwa Zanzibar, imekuwa na mchango
mkubwa katika jitihada za serikali
kuhakikisha huduma za afya kwa wananchi zinakuwa bora pamoja na kuviimarisha
vituo vya afya mijini na vijijini.
Alifahamisha
kuwa kupitia miradi hiyo, huduma za afya ya mama na mtoto ikiwemo kupunguza
vifo vitokanavyo na uzazi zimekuwa nzuri kulinganisha na siku
zilizotangulia.
Aidha, alisema
kufanikiwa kwa mradi wa kupambana na ugonjwa wa malaria unaofadhiliwa na
taasisi ya Clinton Foundation inayoongozwa na Rais mstaafu wa Marekani Bill
Clinton, ni kielelezo cha faida itokanayo na juhudi za nchi hiyo.
Kwa upande wa
maambukizi ya virusi vinavyosababisha UKIMWI, Naibu Waziri huyo alisema
kumekuwa na mwamko mkubwa kwa wananchi kujitokeza kupimwa afya zao na kupatiwa
ushauri nasaha.
Alisema
kumekuwa na ongezeko kubwa la watu kupima afya zao kwa ajili ya kuangalia
maambukizi hayo, kutoka watu 13,000 mwaka 2005 na kufikia 80,000 mwaka 2013.
Aidha alieleza
ingawa vijana wanaotumia dawa za kulevya wanaendelea kujidunga sindano, lakini
wamepata uelewa mkubwa na kuacha kutumia sindano moja kwa watu wengi, na hivyo
kusaidia kupunguza maambukizi ya maradhi ya UKIMWI.
"Mbali na
mafanikio hayo, pia misaada ya Marekani imetuwezesha kusambaza elimu kwa
wananchi juu ya mambo mbalimbali ya afya, ikiwemo kuwahamasisha akinamama wajawazito
kujifungulia nyumbani, na wengi wameitikia wito huo", alisema.
Alieleza
matumani yake kuwa, katika ziara yao wajumbe hao wataona na kuridhishwa na
hatua iliyopigwa, ili ziara yao iwe chachu kwa Zanzibar kuendelea kunufaika na
misaada ya Marekani.
Alisema
serikali ya Zanzibar inathamini uhusiano mzuri na wa karibu kati yake na
Marekani, kwani umelenga kustawisha hali za wananchi wa pande hizo na kuzidi
kushirikiana.
Naye Naibu
Mkurugenzi wa taasisi ya Path Finder International Dk. Pasien Stephen Mapunda
kutoka Tanzania ambaye anafuatana na ujumbe huo, alisema ziara yao itawafikisha
katika hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja kujionea maendeleo
yaliyofikiwa. Maeneo mengine watakayofika ni baadhi ya nyumba za kubadilisha
tabia kwa vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya (Sober Houses), Zayedesa
na 'Key Population Network iliyoko Miembeni mjini Zanzibar, na makundi kadhaa
hatarishi.
No comments:
Post a Comment