WAFANYAKAZI
120 wa kampuni ya simu za mkononi ya Zantel kutoka Zanzibar wako hatarini
kufukuzwa kazi.
Akichangia
bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu hivi karibuni,Mwakilishi wa Wete
mwezi uliopita, Asaa Othman Said alisema nyaraka za wafanyakazi zinazoagiza
kufukuzwa tayari zimeandaliwa baada ya Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo kusema
hapendi kufanya kazi na Wazanzibari kwa sababu ni wavivu.
Aliiomba
Wizara kuingilia kati kuhakikisha maslahi ya Wazanzibari yanalindwa na kuchukua
hatua kuzuia wafanyakazi hao kufukuzwa.
“Nimekasirishwa na kauli ya CEO wa Zantel hasa
baada ya kusema ‘I don’t like
Zanzibaris because are vey lazy’ (siwapendi Wazanzibari kwa wavivu),” alisema Asaa.
Asaa alisema
siku za nyuma aliwahi kuonya hatari ya kampuni hiyo kuhamishiwa Tanzania Bara
kwa kisingizio cha kufuata soko kubwa zaidi.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee
alikiri hilo na kusema amefanya mazungumzo na uongozi wa Zantel kuhakikisha
hilo halitokei.
Aidha alisema
Waziri anaeshughulikia na ajira, Haroun Ali Suleiman nae amefanya mazungumzo na
uongozi wa Zantel kuhusu sakata hilo, lakini hakuweza kutoa ufafanuzi kwa kuwa
wakati huo hakuweko barazani.
Mzee alisema
atahakikisha maslahi ya Zanzibar kutoka ndani ya kampuni hiyo yanalindwa na
kumuonya Mtendaji mpya wa kampuni hiyo kutohamisha kodi kuipeleka Tanzania
Bara.
“Nilimtaka ahakikishe kile kinachofanywa na
Mtendaji anaeondoka na yeye anakifanya na asijaribu kuhamisha kodi kupeleka
Tanzania Bara,” alisema.
Mzee aliwahakikishia
Wawakilishi kumuachia yeye suala hilo na kwamba atalishughulikia kwa nguvu
zote.
Hata hivyo,
Mwanasheria wa kampuni hiyo, Salum Taufiq alikanusha akisema hakuna mfanyakazi
aliefukuzwa kazi isipokuwa wafanyakazi 113 wamemaliza mkataba ambao uliokuwa
muda wa miezi sita.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi, Taufiq alisema kampuni ina mikataba ya kudumu na ya
muda kwa mujibu wa sheria za ajira, kutokana na hali hiyo wafanyakazi hao ambao
waliokuwa walinzi wa minara baada ya kumaliza mkataba Disemba 31 hawakupewa
mkataba mwengine.
Aidha alisema
lengo la kampuni ni kubakia na wafanyakazi ambao watakuwa wanahusika na
shughuli za msingi za mawasiliano, lakini pia haina maana ya kukiuka sheria na
haki za mtu yoyote.
Pia alisema
kesi hiyo ipo mahakamani hivyo ni vyema kusubiri maamuzi ya mahakama.
No comments:
Post a Comment