Na Ikulu (Sri Lanka)
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali imedhamiria kukabiliana na maradhi ya
mazao likiwamo zao la mnazi ambalo linakabiliwa na tatizo la mnyauko.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa ni muhimu kwa Serikali kuchukua hatua za kukabiliana
na tatizo la minazi kwa sababu watu wengi katika baadhi ya maeneo ambayo uchumi
wake unategemea zao la mnazi wanakabiliwa na hatari ya kweli kweli ya
kuathirika kwa maisha yao .
Rais
Kikwete ametoa uhakikisho huo jana, Jumamosi, Novemba 16, 2013, wakati
alipokutana na Waziri wa Maendeleo ya Minazi na Maendeleo ya Shamba la Janatha
wa Sri Lanka , Mheshimiwa
Jagath Pushpakumara na ujumbe wake mjini Colombo .
Waziri huyo aliandamana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti ya Minazi ya Sri Lanka .
Rais
Kikwete yuko nchini Sri
Lanka kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi
Wanachama wa Jumuia ya Madola (CHOGM) unaomalizika leo, Jumapili, Novemba 17,
2013. Mkutano huo wa siku tatu, ulianza juzi, Ijumaa, Novemba 15, 2013.
Mheshimiwa
Pushpakumara na ujumbe wake walikuwa wanamwelezea na kumkabidhi Rais Kikwete
Ripoti ya Magonjwa ya Minazi iliyoandaliwa na wataalam wa minazi wa Sri Lanka
ambao walitembelea Tanzania Julai mwaka huu.
Wataalam
hao walitembea Tanzania
na kufanya utafiti kuhusu ugonjwa unaolikabili zao la minazi kufuatia ahadi ya
Rais Mahinda Rajapaksa aliyoitoa kwa Rais Kikwete wakati alipofanya ziara rasmi
ya Tanzania Juni 27, 2013, na baadaye kushiriki katika Mkutano wa Smart
Partnership Juni mwaka huu.
Rais
Rajapaksa alitoa ahadi hiyo baada ya kuelezwa na Rais Kikwete kuhusu zao la
kukauka kwa minazi nchini. Mnazi ni zao muhimu sana
katika uchumi wa Sri Lanka
na ni zao tegemeo kwa wananchi wa Taifa-Kisiwa hilo
kilichoko kusini mashariki mwa India
katika Barahri ya Hindi.
Wataalamu
waliofuatana na Waziri huyo wamemwambia Rais Kikwete kuwa ugonjwa unaolikabili
zao hilo la minazi ambao pia unashambulia minazi
katika eneo la Caribbean hauna tiba kwa sababu
mpaka sasa hakuna taasisi yoyote ya utafiti imegundua dawa hiyo.
Wataalam
hao ambao walikaa Tanzania kwa wiki moja, zikiwamo siku mbili katika Zanzibar,
wanasema kuwa zao hilo la mnazi, kama ilivyo katika nchi nyingine zinazolima
zao hilo, lina uwezo mkubwa wa kusaidia uchumi kupitia viwanda vidogo vidogo.
Wakati
wakiwa Tanzania , wataalam
hao wa Sri Lanka
walifanya uchunguzi na utafiti kwa karibu na wataalam wa Taasisi ya Utafiti ya
Kilimo ya Mikocheni (MARI).
No comments:
Post a Comment