Na Mohammed Muombwa Seattle Washingtoni USA
Wakati huu Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd akiwa katika ziara ya kikazi mjini Seattle Marekani, Mwandishi Mohamed Muombwa anatuletea makala fupi ya Mji wa Seattle kwa lengo la kuwapa nafasi wananchi waliopo nyumbani kujifunza japo jambo moja kutoka Mji huu wa mvua.
Seattle ni miongoni mwa miji maarufu iliyomo katika jimbo la Washingon. Jina la kupanga la mji huu ni "Mji wa Malkia wa Marekani" Hakuna malkia mbaya duniani, au siyo? Wakaazi wapatao 3.4 milioni wanaishi hapa.
Hapa zamani za kale walowezi wa kizungu waliovamia mji huu waliupachika jina la New York, lakini jina hili hatimaye likapikuliwa na jina la kiongozi wa Wahindi Wekundu aitwae Sealth. Wahindi Wekundu ndio wenyeji wa asili wa Seattle. Kwa hivyo asili ya jina la seattle inatokana na jina la kiongozi wa Wahindi Wekundu.
Kiuchumi: Seattle imepitia mikondo mingi ya mabadiliko ya kiuchumi. Imeanzia na uchumi wa uharibifu wa mazingira wa kukata miti na kuiuza nchi za nje. Kutoka biashara ya magogo ya miti Seattle ikaingia katika uchumi wa kutengeneza meli kwenye karne ya 19. Umaarufu wa Seattle ukapanda tena kilima baada ya uwekezaji wa kutengeneza ndege za aina ya "Boeing" kuhamia hapa kwenye miaka ya 1980. Uwekezaji huu unatoa ajira zaidi ya 20,000 katika kada mbali mbali. Mageuzi mengine ya kiuchumi yaliyoipandisha chati Seattle kiuchumi ni uwekezaji katika teknologia ya mawasiliano. Kampuni maarufu ya Microsoft inayomilikiwa na tajiri mkubwa duniani bwana Bill Gates inaendesha shughuli zake nyingi hapa. Kwa kifupi mji wa Seattle unanukia kikompyuta kompyuta kila chochoro unayopita. Aidha tajiri huyu amefungua afisi yake inayojishughulisha na kupambana na ukimwi ijulikanayo Bill Gates Foundation.
Uchumi wa Seattle hivi sasa umeingia katika mkondo wa uchumi endelevu wa kijani. Uchumi huu hujali mno utunzaji wa mazingira.
Kimandhari: Seattle ni mji wa Mvua. Mawingu meusi huonekana kila mara yakivinjari huku na kule. Kama Waingereza kwao wakati wowote ni wakati wa chai, hapa Seattle wakati wowote ni wakati wa mvua. Mji wa Seattle umejengwa milimani. Wakaazi wa hapa wanatoka karibu mabara yote; wapo Waafrika, wahindi, wazungu kutoka nchi za Scandanavia, Wayahudi, Waarabu. Ndugu zetu kutoka Zanzibar ni wengi kiasi hapa. Kwa hivyo utembeapo mjini utakutana na rangi za watu tofauti ambazo hutoa mandhari nzuri ya mji huu.
Kauli mbiu: Mji wa Seattle unaongozwa na watu wanaojua nini wanakitafuta kwa maslahi ya wakaazi wake. Kauli mbiu ya Seattle ni: Mji wa nia njema. Uchaguzi wao huu ni shabash kweli kweli kwani waswahili husema "Nia njema hairogwi" Kauli mbiu ya mji wetu wa Zanzibar ni ipi? Hatuoni kama ipo haja nasi kuwa na Kauli mbiu?
Wimbo wa Mji wa Seattle: Mji huu unawimbo wake ambao maneno yake yamepangika kama yale mashairi yaliyotungwa na washairi wa Mangapwani akina mwalimu Buda. Wimbo huu unasaidia wakaazi kujenga mahaba zaidi na mji wao. Hebu soma kipande hiki kidogo:
Mji wa Seattle umeketi kwenye milima saba
Utukufu wake umeenea
Kwenye miguu yake kuna Puget Sound (jina la pahala) n.k
Hatuoni nasi tuna haja ya kuwa na wimbo wetu wa mji wa Zanzibar? Wimbo wa mji ukifundishwa maskulini mwetu unaweza kusaidia vizazi vyetu kuupenda mji wao
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Atembelea Mgodi wa Elianje Genesisi Uliopo
Namungo Ruangwa na Kuzungumza na Wananchi Tumedhamiria Kuwainua Kiuchumi
Wachimbaji Wadogo
-
Waziri Mkuu na Mbunge wa Ruangwa , Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi
katika Uwanja wa Namango wilayani Ruangwa
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema ...
32 minutes ago
No comments:
Post a Comment