Na Kadama Malunde,Shinyanga
MCHIMBA madini ya dhahabu aliyejulikana kwa jina la Emmanuele Chacha (29), ameuawa kwa kuchomwa
kisu kifuani na mwanamme mwenzie katika ugomvi wa kugombea mwanamke uliotokea
kijiji cha Kalole kata ya Lunguya wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, SACP
Evarist Mangala kwa vyombo vya habari,
tukio hilo limetokea Januari 10 mwaka huu saa tano usiku.
Alisema marehemu ambaye ni
mchimbaji mdogo wa madini aina ya dhahabu mkazi
Nyangalata wilayani Kahama mwenyeji wa Tarime mkoani Mara, aliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani na mchimbaji
mwenzake, Cosmas Mazigo (23) wakati wakigombea mwanamke mmoja.
Kamanda Mangala alikitaja chanzo cha mauaji hayo kuwa ni ugomvi wa
kugombea mwanamke ambaye bado hajafahamika, kitendo ambacho kilisababisha
marehemu kuchomwa kisu kifuani.
Wakati huo huo katika kijiji cha Mwendakulima wilayani Kahama
mwendesha pikipiki maarufu bodaboda
aliyejulikana kwa jina la Ally Tibaijuka (25), mkazi wa Nyasubi mjini
Kahama amenusurika kufa baada ya kupigwa risasi moja ya bega la kulia na mteja
wake aliyemfahamu kwa sura.
Kamanda Mangala alisema, tukio hilo limetokea Januari 11 mwaka huu saa
10 alfajiri baada ya mteja huyo kumwomba mwendesha pikipiki huyo ampeleke
kijiji cha Mwendakulima kutoka eneo la klabu ya usiku iitwayo Social Club
lakini ghafla mtu huyo alimpora pikipiki hiyo yenye namba za usajili T515 CFZ
aina ya SANLG yenye rangi nyekundu mali ya Rashid Ramadhan.
Alisema mbali na kumpora pikipiki pia alipora fedha taslimu shilingi
25,000 pamoja simu moja aina ya TECNO yenye thamani ya shilingi 75,000 na
kuongeza kuwa katika eneo la tukio imeokotwa bastola moja aina ya browning
yenye namba A558563 ikiwa na risasi moja ambayo imesajiliwa nchini kwa namba TZ
CAR 95579.
Kamanda huyo alisema chanzo cha tukio hilo ni kuwania mali na
kwamba majeruhi amelazwa hospitali ya wilaya ya Kahama na
hali yake ni mbaya na juhudi za kumtafuta mtuhumiwa zinaendelea.
No comments:
Post a Comment